1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUkraine

Ukraine yashambulia Crimea kwa droni

17 Mei 2024

Mashambulizi makubwa ya droni yaliyofanywa na Ukraine katika rasi ya Crimea mapema leo, yamesababisha umeme kukatika katika mji wa Sevastopol.

https://p.dw.com/p/4fyhV
Ukraine - Kharkiv
Wanajeshi wa Ukraine wakikagua droni kabla ya kufyatua. Mei 15, 2024.Picha: Inna Varenytsia/REUTERS

Mashambulizi hayo ya droni yaliashiria jaribio la Ukraine la kujibu mashambulizi ya Urusi kaskazini mashariki mwa Ukraine, ambayo yameongeza shinikizo kwa vikosi vya Ukraine ambavyo vimezidiwa idadi na nguvu, mnamo wakati vinasubiri kuwasilishwa silaha muhimu kutoka kwa washirika wake wa magharibi. Ukraine haijatoa tamko lolote kuhusu shambulizi hilo wala kukiri kuhusika kwake.

Kulingana na wizara ya Ulinzi ya Urusi, mifumo yake ya ulinzi wa anga ilidungua droni 51 za Ukraine katika anga ya Crimea. Pia ilidungua droni nyingine 44 katika anga ya jimbo la Krasnodar na sita katika jimbo la Belgorod.

Wizara hiyo imeongeza kuwa ndege za kivita za Urusi na boti zinazoshika doria pia ziliharibu droni sita katika Bahari Nyeusi.

Soma zaidi: Zelensky: Hali ya utulivu imeanza kurejea katika mkoa wa Kharkiv

Mikhail Razvozhayev, gavana wa jimbo la Sevastopol, ambako ndiko iliko kambi kubwa ya zana za kijeshi za Urusi katika Bahari Nyeusi, amesema shambulio hilo la droni liliharibu kituo cha nguvu ya umeme cha mji huo. Alisema inaweza kuwachukua siku nzima ili kurejesha umeme. Aidha aliongeza kuwa shule katika mji huo zitafungwa kwa muda.

Ukraine yalenga vituo vya mafuta na nishati vya Urusi

Awali, mashambulizi ya Ukraine yaliharibu ndege na hifadhi ya mafuta karibu na kambi ya jeshi la anga ya Belbek iliyoko karibu na Sevastopol. Hayo ni kwa mujibu wa picha za satelaiti zilizochapishwa na kampuni ya Maxar Technologies.

Fahamu zaidi kuhusu mzozo wa Ukraine

Katika jimbo la Krasnodar, maafisa wamesema shambulizi la droni mapema leo Ijumaa, yalisababisha moto katika kiwanda cha kusafisha mafuta cha Tuapse. Moto huo ulizimwa baadaye na hakuna aliyeuawa.

Ukraine imekuwa ikishambulia vituo vya mafuta na miundombinu nyingine ya nishati ndani ya Urusi na kusababisha uharibifu mkubwa.

Soma pia: Urusi yaendeleza mashambulizi zaidi kwa Ukraine

Droni za Ukraine pia zilishambulia bandari kuu katika Bahari Nyeusi ya Novorossiysk.

Hayo yakijiri, vikosi vya Ukraine vilikuwa vikijitahidi kuwazuia wanajeshi wa Urusi kusonga mbele katika jimbo la kaskazini mashariki, Kharkiv, kufuatia msukumo wao ulioanza wiki tatu ziliziopita.

Mji wa Vovchansk, ulioko kilomita 5 tu kutoka mpaka wa Urusi, umekuwa mahali pa mapambano makali katika siku za hivi karibuni.

Mapigano yachacha Kharkiv

Maafisa wa Ukraine tayari wamewahamisha takriban raia 8,000 kutoka mji huo.

Mbinu ya kawaida ya jeshi la Urusi ni kushambulia miji na vijiji kwa mashambulizi ya angani na kuviharibu kabla ya vikosi vyake kuvidhibiti.

Kutibu majeraha yaliosababishwa na vita Ukraine

Katika tukio jingine, Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani Annalena Baerbock amesema Ukraine inahitaji zaidi makombora ya masafa marefu, kupambana na uvamizi wa Urusi katika jimbo lake la kaskazini Kharkiv.

Soma pia: Ujerumani na nchi za Nordic zaahidi kuendelea kuiunga mkono Ukraine

Akizungumza pembezoni mwa mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa Ulaya mjini Strasbourg, Baerbock amesema ni muhimu kukata njia za usambazaji silaha za Urusi na kuipa Ukraine silaha "zinazoweza kutumika kwa masafa ya kati na marefu, na kwamba kwa ushirikiano na washirika wengine, wanafanyia hiyo kazi.

Vyanzo: APE, RTRE