Ulaya na Afrika ya Kusini zakutana
15 Septemba 2011Mkutano huu unakusudiwa hasa kumulika mafungamano ya kiuchumi baina ya Afrika ya Kusini na Ulaya kupitia mikataba mipya ya kibiashara baina yao.
Biashara baina ya pande hizi mbili inatajwa kuwa ni kubwa sana, maana mwaka jana peke yake, Afrika ya Kusini ilisafirisha kupeleka barani Ulaya bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 30, huku ikiingiza bidhaa zinazokadiriwa kufikia thamani ya dola bilioni 25.
Pande hizi mbili zingali zinajadiliana kuhusiana na mipango ya biashara huria baina yao, ingawa pamekuwapo na vikwazo kadhaa, yakiwemo masuala ya fursa za kulifikia soko.
Ujumbe wa Afrika ya Kusini kwenye mkutano huu unaongozwa na Rais wa nchi hiyo, Jacob Zuma, huku ule wa Ulaya ukiongozwa na Rais wa Baraza la Ulaya, Herman Van Rompuy na Rais wa Kamisheni ya Ulaya, Jose Manuel Barosso.
Lakini mkutano huu haugusii masuala ya biashara tu. Kuna mambo muhimu ya kisiasa yanayohusiana na maendeleo ya karibuni katika nchi za Kaskazini ya Afrika, Sudan na Zimbabwe, ambayo pande zote mbili zina maslahi nayo.
Kabla ya mkutano huo kuanza, saa moja iliyopita, mwanadiplomasia mmoja wa Ulaya aliwaambia waandishi wa habari na hapa namnukuu: "Tutagusia umuhimu wa kufanya kazi pamoja, licha ya kuwa mitazamo yetu si kila mara inafanana". Mwisho wa kumnukuu.
Moja ya masuala yanayozigawa pande hizi mbili ni lile la Libya, ambapo siku zote Afrika ya Kusini imekuwa na msimamo wa kukosoa mashambulizi ya Jumuiya ya Kujihami ya NATO yaliyosaidia kumuondoa kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi, huku Umoja wa Ulaya ukiyaunga mkono.
Hadi sasa, Rais Zuma amekataa kulitambua Baraza la Mpito nchini Libya kuwa wawakilishi halali wa watu wa Libya, licha ya waasi hao kumfurusha madarakani Gaddafi.
Suala la mazingira na mabadiliko ya tabia nchi limo pia katika ajenda za mkutano huu kati ya Ulaya na Afrika ya Kusini, hasa kutokana na ukweli kwamba Afrika ya Kusini itakuwa mwenyeji wa mkutano ujao wa Umoja wa Mataifa kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, huko mjini Durban.
Kabla ya mkutano wa leo kuanza, Umoja wa Ulaya ulitangaza msaada wa dola milioni 17 na nusu kwa ajili ya mapambano dhidi ya ugonjwa wa Ukimwi na virusi vinavyosababisha ugonjwa huo na kifua kikuu nchini Afrika ya Kusini.
Mwandishi: Mohammed Khelef/DPA
Mhariri: Josephat Charo