Ulaya yajitetea mkutano wa G20
19 Juni 2012Mataifa ya Ulaya yanajitetea kuwa hayahusiki na hali ya sasa ya kudorora kwa uchumi wa dunia.
Viongozi wa mataifa yenye uchumi mkubwa duniani wanataka kujiweka katika hali kwamba wako pamoja nyuma ya juhudi za kuimarisha ukuaji wa uchumi wa dunia pamoja na kutengeneza nafasi za ajira ili kuweza kuufanyia ukarabati uchumi wa dunia ulio tete, na ambao umegubikwa na hofu juu ya mzozo wa kifedha wa mataifa ya Ulaya. Hii ni kwa mujibu wa rasimu ya taarifa ambayo itawasilishwa mwishoni mwa mkutano huo wa kila mwaka wa kundi la G20.
Shutuma dhidi ya Ulaya
Lakini rais wa halmashauri ya umoja wa Ulaya Manuel Barroso jana Jumatatu (18.06) alikanusha vikali kuwa mataifa ya umoja wa sarafu ya euro yanahusika katika kuuporomoa uchumi wa dunia na kwamba mataifa hayo yamechukua muda mrefu kuweza kuchukua hatua za kupambana na hali hiyo.
"Si wanachama wote wa kundi la G20 wanatekeleza demokrasia. Lakini sisi tunatekeleza Demokrasia. Na tunachukua maamuzi yetu kidemokrasia. Baadhi ya nyakati hii ina maana ya kuchukua muda mrefu. Kwa kuwa huu ni muungano wa mataifa 27 ya kidemokrasia, na tunahitaji kutafuta muafaka wa pamoja. Lakini hatukuja hapa kupewa somo kuhusu demokrasia ama jinsi gani ya kuendesha uchumi wetu".
Hakuna hakika , hata hivyo , iwapo maneno ya kutoa uhakika ya viongozi wa kundi la mataifa ya G20 yatatuliza masoko , ambayo mtazamo wake kuhusu jinsi serikali zilivyochukua hatua kupambana na mzozo huu wa madeni , ulionekana kuwa unayasukuma mataifa ya Ulaya karibu na maafa makubwa kila siku. Hapo jana, muda mfupi baada ya uchaguzi nchini Ugiriki hofu ilitulia kuwa nchi hiyo inaweza kujitoa katika sarafu ya euro, na pia hofu kuwa Uhispania iliufikisha uwezo wa kukopa wa uchumi wa nchi hiyo karibu na kiwango cha kuhitaji mpango wa kuiokoa.
Taarifa ya viongozi wa kundi la mataifa ya G20 ni pamoja na lugha ambayo inaonekana kulenga katika kupunguza mzozo wa Uhispania kwa kuwahakikishia wawekezaji kuwa hazina ya Uhispania haitaishia kutumia gharama za mkopo wa euro bilioni 100 za kuyanusuru mabenki ya nchi hiyo uliotangazwa mwezi huu. Hofu kuwa jukumu la kulipa fedha hizo litaiangukia serikali imesaidia kupandisha gharama za kukopa nchini Uhispania kuwa juu ya kiwango cha asilimia 7.
Umuhimu wa kuchochea ajira
Pia taarifa hiyo inaliweka kundi la G20 katika upande wa wale ambao walikuwa wanadai kuwepo mtazamo wa kuunda nafasi za ajira, ikiwa ni pamoja na kupitia matumizi ya serikali, badala ya kubana matumizi ya bajeti pamoja na kupunguza matumizi ya serikali, hali ambayo inahimizwa zaidi na kansela wa Ujerumani Angela Merkel.
Kansela Angela Merkel anataka kutoka katika mkutano huo wa Los Cabos mpango maalum wa utendaji, ambao utachochea ukuaji wa uchumi.
"Hapa kila bara linapaswa kutoa mchango wake ambapo hadi sasa kama mataifa ya Ulaya tumetakiwa kufanya. Tutachukua msimamo wa pamoja , kwamba matatizo tuliyonayo katika kanda ya euro, ambayo ni pamoja na matatizo ya ukuaji wa uchumi , tutapambana nayo , kwa kufanya mageuzi ya kiuchumi, kubana matumizi katika bajeti, na pia kuchochea ukuaji wa uchumi".
Rais Barack Obama wa Marekani amejaribu kutoa uhakikisho kuwa mataifa ya Ulaya yako karibu na kuchukua hatua sahihi kupambana na mzozo wa kifedha ambao utatuliza masoko na kuyaweka matatizo ya bara hilo mbali na kuuharibu uchumi wa dunia.
Mwandishi : Bergmann, Christina / ZR/ ape / Sekione Kitojo
Mhariri : Mohammed Abdul Rahman