Ulimwengu usifeli Iran kama ulivyofeli Korea Kaskazini, IAEA
17 Oktoba 2023Mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti matumizi ya nishati ya nyuklia (IAEA) Rafael Grossi, amesema ulimwengu haupaswi kushindwa nchini Iran kama ulivyoshindwa nchini Korea Kaskazini ambayo iliwafukuza wachunguzi wa kimataifa wa shirika hilo, na sasa inaunda silaha za nyuklia.
Kulingana na Grossi, vifaa vya ziada vya ufuatiliaji shughuli za nyuklia chini ya mkataba wa kimataifa kati ya Iran na mataifa yenye nguvu duniani, vimeondolewa Iran kufuatia amri ya nchi hiyo, na sasa IAEA haiwezi kukagua kwa haraka maeneo ambayo hayajatangazwa.
Amesisitiza kuwa shirika lake la IAEA ndiyo macho na masikio ya jamii ya kimataifa kwa sasa nchini Iran.
Kwenye ujumbe wake kwa mkutano wa kila mwaka wa Marekani kuhusu udhibiti wa silaha uliofanyika jana, Grossi amesema ana wasiwasi mkubwa kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Shirika la IAEA halijaweza kuingia Korea kaskazini tangu nchi hiyo ilipowatimua maafisa wake mwaka 2009, na sasa shirika hilo linaona tu kwa mbali maendeleo ya nchi hiyo ya nyuklia.