1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu walaani shambulio la treni inayounganisha India na Pakistan

Oummilkheir20 Februari 2007

Mpakistan mmoja anahojiwa na mabaniani wawili wanasakwa na polisi nchini India

https://p.dw.com/p/CHJo
Treni ya "urafiki" inafuka moto.
Treni ya "urafiki" inafuka moto.Picha: AP

Ulimwengu mzima umelaani mashambulio ya mabomu dhidi ya “treni ya urafiki”-“SAMJHAUTA EXPRESS “inayoiunganisha India na Pakistan na kuhimiza utaratibu wa amani uendelezwe.Raia mmoja wa Pakistan anahojiwa na polisi ya India.

Usman Mohammed,mkaazi wa Karachi,alikua ndani ya toto moja la treni “SAMJHAUTA EXPRESS ambako miripuko iligunduliwa baada ya matoto mawili kuripuliwa na kugharimu maisha ya watu wasiopungua 68,usiku wa jumapili kuamkia jana jumatatu .

Inspekta wa polisi katika jimbo la kaskazini mwa India, Haryana –Sharad Kumar ameuambia mkutano pamoja na waandishi habari ,raia huyo wa Pakistan angali bado anahojiwa.

Polisi imechapisha picha za watuhumiwa wawili wengine wanaosemekana walipandia new-Delhi na kuteremka dakika 15 kabla ya mashambulio kutokea,hata kabla ya treni hiyo kufika kituoni .Wote wawili walikua wakizungumza kibaniani.

Ulimwengu mzima umelaani mashambulio hayo.Katibu mkuu wa Umoja wa mataifa Ban Ki-Moon amesema “hakuna lolote linaloweza kuhalalisha uhalifu kama huo.Ameshadidia wahusika lazma wafikishwe mahakamani.

Hata hivyo katibu mkuu wa Umoja wa mataifa amesema ameridhishwa na azma ya viongozi wa India na Pakistan ya kuendeleza utaratibu wa amani.

Laana zimetolewa pia na viongozi wa Marekani mjini Washington. Msemaji wa ikulu ya Marekani David Almacy amesifu uongozi wa waziri mkuu Manmohan Singh wa India na Pervez Musharraf wa Pakistan akisema mashambulio hayo yamelengwa kufuja maendeleo yaliyopatikana katika utaratibu wa amani kati ya nchi hizo mbili.

Viongozi wa pande zote mbili,India na Pakistan wamelaani mashambulio hayo.Waziri mkuu wa Pakistan Shaukat Aziz amesema mashambulio hayo ya kigaidi yasiachiwe kukorofisha utaratibu wa amani kati ya nchi mbili.

Hoja sawa na hizo zimetetewa pia na wahariri wa magazeti ya India .

“Njia bora pekee ya kuwashinda nguvu magaidi,ni kuhakikisha utaratibu wa amani unaendelea” limeandika gazeti la The Hindu,likishadidia taaarifa zilizotolewa hapo awali na serikali za India na Pakistan.

“Utaratibu wa amani lazma uendelezwe”limesisitiza kwa upande wake gazeti la The Asian Age,linalohisi hata kama hakuna kundi lolote la kigaidi lililodai dhamana,lakini shambulio hilo linabainisha wazi kabisa,waasisi wake wamelenga kufuja utaratibu wa amani.

Ujumbe wa serikali ya Pakistan ukiongozwa na waziri wa mambo ya nchi za nje Khurshid Kasuri unatazamiwa kuwasili New-Delhi leo jioni.Kabla mya hapo mwanadiplomasia huyo wa Islamabad alisema:

“Serikali za India na Pakistan zisiwaachie magaidi kulifikia lengo lao.Kinyume kabisa,tunabidi kuharakisha utaratibu wa amani.Pekee ufumbuzi wa masuala tete yaliyosalia ndio utakaosaidia kusonga mbele.”

Ujumbe huo wa India unakuja New-Delhi kushiriki katika mazungumzo ya kamisheni ya pamoja ya India na Pakistan iliyoundwa mwaka 2004 kwa lengo la kuendeleza utaratibu wa amani.