Ulinzi waimarishwa Kenya mkesha wa uchaguzi
7 Agosti 2017Nchini Kenya leo ni mkesha wa siku ya uchaguzi mkuu na mipango yote kadhalika maandalizi imefikia hatima. Katika ukumbi wa Bomas Of Kenya ambako ndicho kituo kikuu cha kuhesabia kura, ulinzi umeimarishwa na kila atakayekuingia anakaguliwa na kupekuliwa. Hii leo Wakenya wamekuwa wakithibitisha ikiwa majina yao yapo kwenye daftari la wapiga kura katika kila kituo. Wakati huo huo, mshauri mkuu wa kiongozi wa upinzani wa NASA ameikimbia Kenya kwa kuhofia usalama wake.
Yamesalia masaa machache kabla vituo vya kupigia kura kufunguliwa rasmi na mchakato wa kupiga kura kuanza. Tume ya uchaguzi ya Kenya, IEBC, imekuwa mbioni kuhakikisha kila kitu kiko shwari kabla ya siku ya siku. Vifaa vya kupigia kura vimekuwa vikisafirishwa kote nchini ili kuwafikia wapiga kura kwenye vituo vyote 40,883. Mwenyekiti wa IEBC, Wafula Chebukati, anashikilia wako tayari kwa shughuli muhimu ya kesho.
Majina ya wapiga kura yameorodheshwa kwenye nakala za daftari la kupigia kura pamoja na nambari ya kitambulisho. Nambari hizo za kitambulisho zilizoonyeshwa ni ile ya kwanza na ya mwisho. Za katikati zimefichwa kwa alama za nyota ili kuhifadhi maelezo ya mpiga kura.
Nakala hizo zinamuelekeza mpiga kura kuhusu chumba atakachoingia ili kupiga kura kadhalika maelezo ya kituo chenyewe cha kupigia kura. Mgombea wa urais wa Jubilee, Uhuru Kenyatta, na mwenzake William Ruto wanawasisitizia Wakenya kudumisha amani hata baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.
Mitaani raia wamekuwa wakijishughulisha na hatua za mwisho mwisho za kutazama majina yao kwenye daftari la wapiga kura lililobandikwa kwenye vituo vya kupigia kura. Baadhi niliokutana nao walikataa kujitambulisha ila wanaelezea kilichowasibu.
Kwa upande mwengine, upinzani wa NASA umejikuta katika hali isiyoeleweka baada ya mshauri mkuu wa mgombea wao wa urais kukimbilia nchi ya kigeni kwa madai ya kuhofia usalama wake. Salim Lone aliyemshauri mkuu wa kisiasa wa Raila Odinga amekiri kuwa hayupo Kenya kwa kuhofia usalama wake ijapokuwa hajapokea kitisho cha aina yoyote. Mapema Mgombea wa urais wa NASA, Raila Odinga, alimtakia kila mema mpinzani wake mkuu kabla ya siku ya kupiga kura rasmi kesho.
Yote hayo yakiendelea usalama umeimarishwa katika ukumbi wa Bomas of Kenya wakati vituo vinasubiriwa kufunguliwa. Maafisa wa tume ya uchaguzi IEBC pamoja na wangalizi wa uchaguzi wa kigeni na humu nchini watapiga kambi humo kwa siku saba zijazo. Hicho ndicho kituo rasmi cha kuhesabia kura na matokeo yatatangazwa kutokea Bomas Of Kenya. Magari ambayo hayatakuwa na vibandiko maalum vya kuyaegesha yataarimwa kurejea kwenye lango kuu.
Mwandishi: Thelma Mwadzaya/DW Nairobi
Mhariri: Mohammed Khelef