Umaskini wa watoto nchini Ujerumani
8 Agosti 2006Ni saa saba katika kituo hicho cha kanisa katika mtaa wa Jenfeld wa mjini Hamburg, Kaskazini mwa Ujerumani. Watoto wengi wanakimbilia kupewa chakula cha mchana ambacho ni bure kwa watoto kati ya umri wa miaka minne hadi 12. Boris kwa mfano anakuja hapa kila siku. Anasema: "Chakula ni kitamu na pia wazazi wangu wanataka niende hapa."
Wazazi wake Boris hawana ajira. Mara nyingine wanapika nyumbani, lakini chakula cha hapa ni kitamu zaidi. Hana maelezo mengine.
Kituo hicho kimefunguliwa miezi sita iliyopita. Kuna vyumba kadhaa na bustani ambapo watoto wanaweza kucheza. Tayari watoto wengi wanakuja hapa, anasema Thomas Lucht, mfanyakazi wa kituo hiki: “Kila siku watoto 60 hadi 70 huja kwetu. Na kila Alhamisi tunafanya sherehe maalum, hapo takriban watoto 120 hadi 160 wanatutembelea.”
Mwanzoni watoto 15 tu walikuja, lakini baada ya muda wazazi hawakuogopa tena kuonyesha umaskini wao na walianza kuwaleta watoto wao.
Chakula cha leo ni aina ya pasta na mchuzi wa nyanya. Kwa mwenendo mzuri watoto wanapewa sahani zao wakizungumza kwa furaha. Kinachoonekana ni kwamba wengi wao wamenenepa kutokana na chakula kibaya wanachokila kwa kawaida.
Wazazi wana fedha za kuwanunulia watoto wao chipsi au aiskrimu, bado lakini chakula cha kituo hiki cha kanisa ni bure. Na kuna sababu maalum, anaeleza Tobias Lucht: “Tungeweka bei ya Euro moja kwa chakula hicho, watoto wengi hawangekuja. Hata ikiwa wana Euro hii moja, wangeitumia kununua peremende na kuwaonyesha watoto wengine kwamba wana uwezo wa kununua kitu. Umaskini ni neno, lakini lazima kujiuliza umaskini ni nini? Baadhi ya familia hazina fedha, lakini familia nyingine haziwapi watoto umuhimu wa kwanza.”
Kwa sababu hiyo, Tobias Lucht na wafanyakazi wenzake wanaona kwamba kuna umaskini wa hisia: "Kuna watoto wakija hapa siku ya kwanza, wanatung'ang'ania na hawataki kutuacha tena. Ni dalili kwamba hawapewi mapenzi ya kutosha nyumbani.”
Mjini Hamburg kila mtoto mmoja kati ya watoto watano ni maskini na idadi hiyo inazidi kuongezeka.