Umoja wa Afrika wajadili matatizo ya bara hilo
3 Julai 2017Licha ya mada kuu ya mageuzi ya umoja huo,marais na viongozi wa serikali wa nchi 55 ya AU wanatakiwa kumaliza mkutano wao wa siku mbili hapo kesho huku wakitilia mkazo swala la kujitegemea kifedha kupitia ushuru wa bidhaa vinavyoingizwa kutoka nje ya bara hilo.Taarifa kamili na mjumbe wetu maalumu mjini Addis-Ababa. Mwenye kiti wa Umoja wa Afrika na ambae ni rais wa Guineae Alpha Konde alielekeza hotuba yake ya ufunguzi wa mkutano huo katika kile alichokielezea kuwa ni majukumu ya viongozi kuwahakikishia vijana mustakbali mwema."ninaomba kuhakikisha kwamba vijana wetu wamepewa nafasi ilikupanuka kifikra na katika namna nyingine zote.Hatutaki kushuhudia kila siku mauwaji ama vifo vya vijana wetu kwenye bahari kwa ajili ya kutafuta maisha bora mahala kwengine".
Mwenyekiti huyo wa Umoja wa afrika amependekeza kwamba ajira kwa ajili ya vijana iwe ajenda kuu kwenye mkutano wa Novemba mjini Abidjan baina ya Umoja wa Afrika na Umoja wa ulaya. Kwa upande wake rais wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika Mahamat Moussa Faki amesema kwamba wakati umewadia viongozi wa afrika kuungana pamoja ilikukemea vita na machafuko. Faki amesema kwamba mwaka 2018 unatakiwa kuwa ni mwaka wa kunyanyika kwa Afrika kutokana na vita na vilevile kusitisha milio ya risasi, "Tunawasiwasi kutokana na hali ya kiusalama kwenye nchi kadhaa ikiwemo DRC,Sudan Kusini ,Libya na Mali". Rais wa halmashauri ya umoja huo amesema kwamba mtizamo wa marais wa nchi za umoja wa afrika mpya kwa ajili ya mageuzi ya umoja huo,bila shaka unaleta matumaini ya mwanzo mpya.
Kagame kiongozi wakamati ya maeguzi ya kiuchumi
Rais wa Rwanda Paul Kagame ambae ameongoza kamati ya mageuzi ya kiuchumi, na utawala bora kwenye umoja huo amesema kwamba malengo hayo yatakamilika ikiwa waafrika watazungumza kauli moja licha ya tofauti zao. Mkutano huo wa kilele unatarajiwa pia kuzungumzia migogoro ya kikanda mfano wa Libya,Sudan kusini, Mali na jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo . Kuhusu Kongo marais hao wametarajiwa kuunga mkono msimamo wa rais kabila wa kupinga kile anachokielezea kuwa ni uingiliaji kati wa maswala ya ndani ya nchi yake na nchi za magharibi.
Leonard She Okitundu waziri wa mamabo ya nje wa kongo amesema kwamba pendekezo hilo lilidhinishwa kwa kauli moja na mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje."ulipata uungaji mkono mkubwa wa mawaziri wenzetu na tunasubiri huenda baadae leo ama kesho marais kuidhinisha ungwaji mkono huo unaopinga kile tunachoita kuwa ni utawala mambo leo wa wazungu".
Swala jingine muhimu kwenye mkutano huu wa kilele ni kufadhiliwa kwa bajeti na miradi mikubwa umoja wa afrika na wafrika wenyewe kwa hiyo,ushuru wa asilimi 0.2 utatozwa kwa bidhaa zote zinavyoagizwa kutoka nje ya bara hili.
Mwandishi: Saleh Mwanmilongo, Addis Ababa
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman