Umoja wa Afrika wasimamisha uanachama wa Gabon
1 Septemba 2023Siku ya Alhamisi (31.08.2023) baraza la amani na usalama la Umoja huo, lilisema kuwa linalaani vikali mapinduzi hayo yaliomuondoa madarakani rais Ali Bongo. Wiki chache zilizopita, Umoja huo wa Afrika pia ulisimamisha uanachama wa Niger baada ya mapinduzi ya kijeshi ya mwezi Julai.
Soma pia:Viongozi wa Afrika kujibu hatua ya mapinduzi ya kijeshi Gabon
Uanachama wa Burkina Faso, Mali, Guinea na Sudan katika Umoja huo pia umesimamishwa tangu mapinduzi ya kijeshi katika mataifa hayo.
Umoja wa Ulaya wapinga mapinduzi ya kijeshi Gabon
Katika hatua nyingine, mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Josep Borrell, amesema kuwa Umoja huo unapinga kutwaliwa kwa nguvu kwa mamlaka nchini Gabon. Katika taarifa, Borrell amesema kuwa changamoto zinazoikabili Gabon lazima zitatuliwe kulingana na kanuni za sheria, utaratibu wa kikatiba na demokrasia.