Umoja wa Mataifa kuinusuru Sudan Kusini
30 Aprili 2014.Akiwashambulia vikali Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini na kiongozi wa waasi Riek Machar, Kamishna Mkuu wa Haki za Binaadamu wa Umoja wa Mataifa Navi Pillay amesema amefadhaishwa na kile kinachoonekana kuwa kutokuwepo kwa hofu juu ya hatari ya kuzuka baa la njaa nchini humo kulikoonyeshwa na viongozi hao wote wawili.
Kauli hiyo imekuja baada ya Pillay akiandamana na mjumbe maalum wa masuala ya mauaji ya halaiki kuwa na mazungumzo na viongozi hao hasimu ikiwa ni siku moja baada ya Umoja wa Mataifa kutowa wito wa dharura wa kusitishwa mapigano kwa mwezi mmoja kuepusha janga la njaa na maafa ya kibinaadamu.
Pillay amekaririwa akisema uwezekano wa kuzuka njaa nchini kote na utapia mlo utakaowaathiri mamia na maelfu ya watu wao kwa sababu ya kushindwa kwao binafsi kutatuwa tafauti zao kwa amani hakuonekani kuwapa wasi wasi mkubwa.
Kuzuwiya Rwanda nyengine Afrika
Mjumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuzuwiya mauaji ya halaiki Adama Dieng amewaambia waandishi wa habari kwamba wanatakiwa waahidi kwa wahanga wa mauaji ya halaiki kuchukuwa hatua zote zinazowezekana wenye mamlaka nazo kuwalinda raia dhidi ya tukio jengine kama lile la Rwanda ambapo hakuna kisingizio cha kushindwa kuchukuwa hatua.
Amesema katika mkutano na waandishi wa habari ambao pia umehudhuriwa na Pillay kwamba ni jambo la wazi kuwa mzozo huo umechukuwa mkondo wa hatari na raia wamekuwa wakishambuliwa kwa makusudi kwa misingi ya kikabila na uhusiano wao wa kisiasa.
Ziara hiyo ya Umoja wa Mataifa nchini Sudan Kusini ambayo inamalizika leo hii inakuja wakati waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry akiwa ziarani barani Afrika ambapo pia anatazamiwa kuizuru Sudan Kusini.
Shinikizo kukomesha mapigano
Marekani ilikuwa mhusika mkuu katika kuisaidia Sudan Kusini kujipatia uhuru wake na Kerry ambaye awanasili Ethiopia leo hii kuanza ziara yake hiyo anatarajiwa kujaribu kuwashinikiza wasuluhishi katika mazungumzo ya amani yanayofanyika Ethiopia kukomesha mapigano hayo ya Sudan Kusini.
Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miezi minne nchini Sudan Kusini ambayo imejipatia uhuru wake kutoka Sudan hapo mwaka 2011 tayari vimesababisha kuuwawa kwa maelfu ya watu na wengine wanofikia mililoni moja nukta mbili wamelazimika kuyakimbia makaazi yao.
Makubaliano ya kusitisha mapigano yaliosainiwa mwezi wa Januari yako mashakani huku maelfu ya watu wakiwa wamepatia hifadhi kwenye makambi ya Umoja wa Mataifa kufuatia wimbi la mauaji ya kikabila ukiwemo ubakaji, kuwaingiza watoto jeshini kwa nguvu na kufanya mauaji kwenye mahospitali,kanisani na miskitini.
Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP
Mhariri : Josephat Charo