Umoja wa Mataifa unataka hatua za haraka kufanywa ili kupunguza umaskini na njaa
10 Septemba 2004Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Koffi Annan, amesema ya kwamba nchi zenye maendeleo duni ulimwenguni zinapiga hatua muhimu kaytika kupunguza njaa na umaskini. Alisema hayo wakati alipokuwa anapitia malengo yaliyowekwa mwanzo wa karne hii na Umoja wa Mataifa kuhusu kupunguza umaskini na njaa kufikia mwaka wa 2015.
Wakati huo huo Bwana Anna ameonya kwamba kupiga hatua katika nchi hamsini ambazo ni maskini kabisa ulimwenguni halijakuwa jambo rahisi. Kati ya nchini hizo hamsini, thelathini na nne kati yao ni nchi kusini mwa Sahara. Baadhi ya nchi hizi ni kama vile Afghanistan, Bangladesh, Sierra Leone na Zambia.
Bwana Annan aliongeza kuwa mwaka wa 2005 utakuwa muhimu kwa bara la Afrika kwa sababu kumaliza umaskini kutahitaji jitihada kubwa. Alikuwa akitoa hotuba katika mkutano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ambao umemalizika baada ya siku tatu.
Malengo ya Karne mpya yalipitishwa mnamo mwaka wa 2000 katika mkutano wa viongozi wa ulimwengu mjini New York. Malengo hayo yalighusia sehemu nane nazo ni umaskini na njaa, elimu ya msingi, usawa wa jinsia, vifo vya watoto wachanga, afya ya mama waja wazito, mazingira na ushirikiano wa kimataifa kwa sababu ya maendeleo.
Tarehe ya mwisho iliyowekwa kwa malengo haya kutimizwa ni mwaka wa 2015, ni yanahusu kupunguza umaskini na njaa kwa asilimia hamsini.
Bwana Annan anasema kuwa habari njema ni kuwa zaidi ya watu milioni mia mbili mashariki na kusini mwa Asia sasa hawaishi katika hali za umaskini sana.
Idadi ya watoto wanaoandikishwa katika mashule ya msingi huko Marekani Kusini, Karibik na sehemu kubwa ya Asia sasa ni zaidi ya asilimia tisini.
Habari za kusikitisha ni kwamba hali katika nchi maskini kabisa ulimwenguni haijaonyesha mabadiliko yoyote na katika baadhi ya nchi hali imekuwa mbaya zaidi.
Taarifa katika miezi kumi na miwili iliyopita katika nchi maskini zimekuwa sio za kutia moyo. Kwa kutoa mfano mmoja tu, idadi ya watu walioambukizwa ukimwi katika mwaka mmoja uliopita ni juu sana katika historia ya nchi hizi, na hivyo kusababisha wasiwasi kuhusu matumaini ya maendeleo katika maeneo hayo ambayo ni makazi ya mamilioni ya watu.
Lakini kuna wale ambao wanasema kwamba suala la kuyataka mataifa maskini ulimwenguni kutimiza malengo ya maendeleo bila ya kuyasamehe madeni yao ni kuyataka mataifa hayo yashindwe. Baadhi ya nchi kama vile Sierra Leone na Burkina Faso ziko katika hali mbaya zaidi baada ya mradi huo kuanza.
Nchi maskini zinavuta mkia katika maendeleo ulimwenguni zikilinganishwa na nchi tajiri.
Kwa nchi nyingi barani Afrika kama vile Sudan, Sierra Leone, Guinea Bissau na Mozambique, madeni zao ni zaidi ya asilimia mia tano ya mapato yao kutoka mauzo ya nje. Hakuna matumaini ya mataifa kuendelea ikiwa yanatumia mapato yao yote kulipa madeni.
Mashirika yasiyo ya kiserikali, yamefanya kampeni ya nchi maskini kusamehewa madeni yao, yakisema kwamba nchi zenye madeni makubwa hazina matumaini ya kutimiza malengo yoyote ya maendeleo.
Mashirika hayo yanasema kwamba Irak ilisamehewa madeni yake ya zaidi ya dola milioni themanini ili kuisadia nchi hiyo kujengwa upya. Mtindo huo unapaswa kufuatwa ili kuziruhusu nchi maskini duniani kufanya maendeleo.
Katika ripoti yake Annan anasena kuwa malengo ya maendeleo bado yanaweza kutimizwa hata katika nchi maskini kabisa, lakini matumaini ya kufanya hivyo yanaendelea kudidimia kutokana na kutokuwepo na nia ya kisiasa ya kuyatimiza.
Baadhi ya nchi barani Afrika ambazo zinaonyesha kupiga hatua za maendeleo ni kama vile Malawi na Rwanda ambazo zimewapeleka watoto wote shuleni. Tanzania imo katika kundi hilo kwa kutimiza lengo la kuwapa wananchi wake maji huku Uganda na Senegal zikipunguza idadi ya watu wanaoambukizwa ukimwi. Msumbiji pia inakaribia kutimiza lengo lake la kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini humo.
Umoja wa Mataifa umeshutumiwa kwa kutoa jukwaa ambako viongozi wa serikali wanaenda na kutoa hotuba za kupendeza na baadaye kupanda ndege na kurudi makwao kuendela na maisha yao kama kawaida. Umoja wa Mataifa una uwezo unaopewa na mataifa wanachama wake.
Suala la kutoa hotuba na kurejea nyumbani ni kweli kwani viongozi wa nchi tajiri waliahidi kutoa asilimia 0.7 ya pato lao la taifa katika kusaidia nchi maskini. Jumla ya mataifa 24 yalikuwa yameahidi kutoa msaada huo lakini ni Norway, Sweden, Denmark, Uholanzi na Luxembourg ambazo zimetimiza ahadi zao. Mtindo ni huo huo na viongozi wa Afrika pia. Ni wangapi kati yao walirudi nyumbani na kuzungumzia suala la kutimiza malengo ya Umoja wa Mataifa, na mabaraza yao ya mawaziri?