1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa waeleza wasiwasi juu ya Burkina Faso

10 Februari 2022

Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa limeelezea wasiwasi wake juu ya hali nchini Burkina Faso, kufuatia hatua ya kubadilishwa kwa serikali kinyume cha katiba mwezi uliopita.

https://p.dw.com/p/46nbR
USA New York | UN Sicherheitsrat -
Picha: Richard Drew/AP/picture alliance

Hata hivyo baraza hilo halikulitaja tukio hilo kama mapinduzi ya kijeshi ama hata kulilaani kwa uwazi.

Kulingana na toleo la awali la waraka ambao shirika la habari la AFP liliupata, baraza hilo limeutolea mwito utawala wa kijeshi kuratibu mara moja kurejeshwa kwa utaratibu wa kikatiba nchini humo, lakini ombi hilo liliondolewa na Urusi, hii ikiwa ni kulingana na mwanadiplomasia ambaye hakutaka kutambulishwa.

soma zaidi: ECOWAS kutoiwekea vikwazo Burkina Faso

Kwenye azimio ambalo lilipitishwa na wanachama 15 wa baraza hilo aidha limeomba kuachiwa huru kwa rais Marc Christian Kabore pamoja na maafisa wengine wa serikali, lakini pia kupewa ulinzi.

Aidha, limeeleza kuunga mkono juhudi za upatanishi za kikanda ili kusuluhisha mzozo uliopo, baada ya kufunguliwa kwa ofisi ya pamoja ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi, ECOWAS, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa nchini humo.