1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Mataifa wasema machafuko yameongezeka Gaza

29 Novemba 2024

Umoja wa Mataifa umesema ukanda wa Gaza umeingia katika machafuko huku njaa ikiongezeka, uporaji ukikithiri pamoja na kuongezeka kwa vitendo vya ubakaji katika maeneo ya makazi huku utulivu wa umma ukizidi kusambaratika.

https://p.dw.com/p/4naia
Hali ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza
Hali ya kiutu kwenye Ukanda wa Gaza.Picha: Saeed Jaras/Middle East Images/AFP/Getty Images

Baada ya kukamilisha ziara yake hivi karibuni katika ukanda wa Gaza, mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Haki za Binadamu katika mamlaka ya Palestina Ajith Sunghay, amesema Wapalestina wanateseka kwa kiwango kikubwa sana.

Sunghay ameuambia mkutano wa waandishi wa habari mjini Geneva kwa njia ya video kutoka Amman kwamba wakati huu, alishtushwa sana na kukithiri kwa njaa.

Sunghay pia amesema kukosekana kwa utulivu na usalama wa umma kunafanya hali hiyo kuwa mbaya zaidi wakati  uporaji umekithiri pamoja na kupigania rasilimali chache zilizoko.

Mkuu huyo wa ofisi ya Haki za Binadamu ameongeza kuwa wanawake wa umri mdogo, wengi waliokimbia makazi yao mara kadhaa, wamesisitiza kuhusu ukosefu wa maeneo salama au faragha katika hema zao za muda.