Umoja wa Ulaya kuipa Armenia euro milioni 270
5 Aprili 2024Tangazo hilo lilitolewa baada ya mazungumzo juu ya kuimarisha uhusiano na Armenia baina ya Waziri Mkuu wa nchi hiyo, Nikol Pashinyan, Mkuu wa Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen, na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Antony Blinken.
Von der Leyen alisema fedha hizo zitakazotolewa kwa miaka minne ni ishara kwamba Umoja wa Ulaya unasimama pamoja na Armenia.
Soma zaidi: Armenia na Azerbaijan zabadilishana wafungwa wa kivita
"Hatujasahau kuhusu hali mbaya ya Waarmenia wa Karabakh waliokimbia makaazi yao. Hali ya wakimbizi nchini Armenia tunaipa kipaumbele. Tumetoa zaidi ya euro milioni 30 kusaidia wakimbizi tangu Septemba mwaka jana, na tuko tayari kufanya zaidi ili kuufanikisha mchakato wa kudumu wa kuwajumuisha wakimbizi." Alisema mkuu huyo wa Umoja wa Ulaya.
Waziri Mkuu wa Armenia alisema mkutano huo wa siku ya Ijumaa (Aprili 5) mjini Brussels ulithibitisha kuimarika kwa ushirikiano baina ya nchi hiyo na Umoja wa Ulaya pamoja na Marekani.