Umoja wa Ulaya kuisaidia Ukraine kujiunga nao
9 Aprili 2022Tukianzia nchini Ukraine kwenyewe, rais wa Halmashauri kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen hapo jana alimpatia tais Volodymyr Zelensky nyaraka za kuanza mchakato wa taifa hilo kujiunga na Umoja wa Ulaya. Akimkabidhi nyaraka hizo, Von der Leyen amesema huo ndio mwanzo wa safari hiyo.
Soma Zaidi: EU yaungana kuhusu Ukraine, lakini haitatoa uanachama wa haraka
Amesema wako tayari kuisaidia Ukraine kujaza maswali yaliyomo kwenye makaratasi hayo na kuongeza kuwa mchakato huo hautachukua miaka kama ilivyo kawaida na badala yake utachukua wiki kadhaa ili kukamilisha hatua hiyo.
Soma Zaidi: Guterres: Kitisho kwa usalama wa dunia kikubwa zaidi sasa
Von der Leyen aidha amesema hayo kwenye mkutano wa pamoja wa waandishi wa habari kati yake na rais Zelensky mjini Kyiv alipokuwa ziarani pamoja na naibu wake Josep Borrel kwamba ananuia kuwasilisha maombi ya Ukraine kwenye baraza la Ulaya katika kipindi cha majira ya joto ya mwaka huu.
Maafisa hao wa ngazi za juu katika Umoja wa Ulaya ni wa kwanza kwenda nchini Ukraine tangu Urusi ilipolivamia taifa hilo. Von der Leyen pia alizuru mji wa Bucha ambako mamia ya miili ya raia wa Ukraine ilikutwa imezikwa baada ya vikosi vya Urusi kuondoka kwenye mji huo.
Kutoka Bucha, ofisi ya mwendesha mashitaka mkuu imesema karibu watu 67 walizikwa katika kaburi la pamoja karibu na kanisa kwenye mji huo ambako kunagunduliwa miili baada ya wanajeshi wa Urusi kuondoka. Iryna Venediktova amesema jana kwamba miili 18 imetambuliwa hadi sasa, 16 ikiwa na matundu ya risasi. Amesema hiyo inamaanisha kwamba wanajeshi wa Urusi waliwaua raia.
Ofisi yake inachunguza vifo hivyo na matukio mengine dhidi ya raia ili kuangazia iwapo yatakuwa ni uhalifu wa kivita. Umoja wa Ulaya pia unashiriki kwenye uchunguzi huo.
Ujerumani kuachana na nishati kutoka Urusi mapema kuliko ilivyokisiwa.
Nchini Ujerumani, taasisi ya utafiti wa kiuchumi, DIW imesema Ujerumani huenda ikaachana na utegemezi wa nishati inayoingizwa kutoka Urusi wakati wa majira ya baridi ya mwaka huu,. Hatua hiyo itakuwa imefikiwa mapema kuliko matarajio ya awali ya serikali ya kuachana na utegemezi huo katikati ya mwaka 2024 ama baada ya hapo.
Suala ya Ujerumani na Ulaya kuachana na utegemezi wa nishati kutoka Urusi limekuchukua nafasi kubwa tangu Urusi ilipoivamia Ukraine.
Soma Zaidi: Ujerumani yajizatiti kuisaidia zaidi Ukraine
Nchini Slovakia, uamuzi wa serikali yake wa kupeleka mfumo wa kujilinda chapa S-300 nchini Ukraine umewaghadhabisha wanasiasa wa upinzani wakisema hatua hiyo inaliweka hatarini taifa lao ingawa Marekani imesifu uamuzi huo. Mfumo huo wa kujilinda na makombora uliundwa enzi ya Kisovieti.
Waziri mkuu wa zamani na mkuu wa chama cha Smer Robert Fico amesema atatoa mwito wa kuitishwa kwa kikao maalumu cha kujadili kuiondoa serikali iliyoko madarakani, huku kiongozi wa chama cha Hlas Peter Pelegrini akiwatuhumu waziri mkuu Eduard Heger na waziri wa ulinzi Jaroslav Nad kwa kuwadanganya watu wa Slovakia akisema mfumo huo ulikuwa maalumu kwa kulinda mipango ya atomiki ya Slovakia na maeneo ya viwanda.
Mashirika: DPAE/DW/APE