Umoja wa Ulaya, Ujerumani kuisaidia Ugiriki
9 Septemba 2020Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya, Ursula von der Leyen alisema Jumanne usiku kupitia ukurasa wake wa Twitter kwamba amehuzunishwa sana na tukio hilo la moto kwenye kambi ya waomba hifadhi na kuongeza kuwa amemtuma mmoja wa makamu wake, Margaritis Schinas.
Soma pia: Kambi ya wahamiaji Ugiriki yateketea kwa moto
Aliandika, mataifa wanachama wako tayari kusaidia na kipaumbele chao ni usalama wa wale walioachwa bila ya makazi. Maelfu ya waomba hifadhi wameachwa bila makaazi kufuatia moto huo kwenye kambi iliyofurika pomoni ya Moria iliyopo kwenye kisiwa cha Lesbos, nchini Ugiriki.
Mapema Jumatano kulifanyika mkutano usio wa kawaida wa serikali katika kasri la Maximos ambalo ni makazi rasmi ya waziri mkuu wa Ugiriki na baada ya kumalizika kwa mkutano huo msemaji wa serikali Stelios Petsas alisema baadhi ya wawakilishi wa serikali wangezuru kisiwa hicho.
"Waziri wa mambo ya ndani wa Ugiriki Takis Theodorikakos, waziri wa masuala ya uhamiaji na hifadhi Notis Mitarachis na rais wa taasisi ya kitaifa ya afya ya umma, NPHO Panagotis Arkoumaneas watakwenda Lesbos na baada ya tathmini ya hali ilivyo kwenye eneo hilo, watafanya mkutano na waandishi wa habari saa sita mchana huko Mytilene."
Ujerumani kuchukua baadhi ya wakimbizi
Ujerumani tayari imesema itaisaidia Ugiriki baada ya tukio hilo lililosababisha takriban watu 12,600 kukosa makazi. Msemaji wa wizara ya mambo ya ndani Steve Alter ameandika kupitia twitter kwamba hatua hiyo inafuatia majadiliano ya kina na serikali ya Ugiriki tangu jana.
Baadhi ya majimbo ya Ujerumani kama Berlin tayari yamesema yatawachukua wahamiaji hao, lakini msemaji huyo hakueleza wazi iwapo waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer ataruhusu hilo.
Soma pia: Wakimbizi wajazana kuvuka mpaka kati ya Uigiriki na Uturuki
Awali waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani ambayo ni rais wa sasa wa Umoja wa Ulaya Heiko Maas alisema wako tayari na kutaka kuangazia mara moja namna watakavyoisaidia Ugiriki.
Maas ameandika kupitia ukurasa wa twitter kwamba hatua hizo zitajumuisha mataifa yaliyo tayari kugawana wakimbizi miongoni mwa walioathirika. Operesheni kubwa ya uokozi ilikuwa inaendelea hii leo katika kambi hiyo.
Wito umetolewa kwa mataifa wanachama wa Ulaya kuingilia kati kusaidia kuwatafutia makazi wakimbizi. Brussels imetangaza kuwasaidia watoto 400 na vijana miongoni mwa wakazi 12,000.
Mzozo wa Moria unaelezea mahitaji ya mageuzi katika sera ya uhamiaji ya Ulaya, mchakato uliozorota kwa muda mrefu kutokana na mgawanyiko baina ya serikali za mataifa wanachama.
Chanzo: Mashirika