Umoja wa Ulaya wakataa mapendekezo ya May kuhusu Brexit
21 Septemba 2018Uingereza ikiwa inatarajiwa kujitoa katika Umoja wa Ulaya Machi 29 mwakani, kuna wasiwasi kwamba makubaliano juu ya uhusiano wa kibiashara wa baadae huenda yasifikiwe katika muda uliopangwa.
Viongozi wote, akiwamo Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May wanatafuta njia ya kutatua suala zito kuhusu mchakato wa Brexit ambalo ni jinsi ya kuhakikisha bidhaa zinaendelea kuingizwa na kutoka kati ya Ireland Kaskazini ambayo ni sehemu ya Uingereza na Jamhuri ya Ireland ambayo ni nchi mwanachama wa Umoja wa Ulaya.
Wakati walipokutana kwa siku mbili katika mkutano wa kilele uliomalizika jana mjini Salzburg Austria, Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Donald Tusk amesema baadhi ya sehemu za mpango wa May wa Brexit - uliopewa jina la Chequers -hazitokubalika.
"Wakati wa kudhihirika ukweli kuhusu makubaliano ya Brexit utakuwa katika Baraza la Umoja wa Ulaya la mwezi Oktoba. Oktoba tunatarajia maendeleo ya kiwango cha juu na makubaliano katika mazungumzo ya Brexit," amesema Donald Tusk.
Viongozi hao wa nchi za Umoja wa Ulaya wametumia siku mbili kujaribu kufikia makubaliano, lakini mazungumzo yao yamegonga ukuta. Kila upande ukijaribu kumshinikiza mwenzake. Huku Umoja wa Ulaya ukiionya Uingereza mara kwa mara kwamba muda unazidi kuyoyoma.
Tusk amesema sehemu muhimu za mapendekezo ya Uingereza katika mpango wake wa kujitoa zitaathiri mataifa 27 yaliyobakia katika Umoja wa Ulaya.
Uingereza haiwezi kuchagua inachokitaka na isichokitaka katika soko la pamoja
May anataka Uingereza ibaki katika soko la pamoja la Umoja wa Ulaya, lakini kwa mauzo ya bidhaa pekee na sio biashara za utoaji wa huduma. Lakini Umoja wa Ulaya umekuwa ukisisita kwamba Uingereza haiwezi kuchagua inachokitaka na isichokitaka ikiwa itabaki katika soko la pamoja.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amesema mapendekezo ya May hayakubaliki hasa katika suala la kiuchumi kwa sababu hayaheshimu uadilifu wa soko moja.
May pia amesema Uingereza na Umoja wa Ulaya wamekubaliana juu ya haja ya uhakikisho wa kisheria kuwa hakutakuwepo na mpaka kati ya Uingereza na Ireland. Lakini Uingereza imelikataa pendekezo la Umoja wa Ulaya la kuibakisha Ireland Kaskazini ndani ya mfumo wa ushuru wa forodha wa umoja huo pale Uingereza itakaposita kuwa mwanachama.
Majadiliano na viongozi wa mataifa ya Umoja wa Ulaya sio tatizo pekee analokabiliana nalo May kwa sasa. Mpango wake huo wa Chequers unakosolewa hata ndani ya chama chake cha Conservative. Baadhi ya wanachama wenzake wanasema Uingereza itafungika katika Umoja wa Ulaya na haitoweza kuwa na makubaliano ya kibiashara na mataifa mengine ulimwenguni.
Mwandishi: Yusra Buwayhid/ap,afp
Mhariri: Daniel Gakuba