1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya wakusanya fedha kukabiliana na COVID-19

4 Mei 2020

Umoja wa Ulaya umeitisha mkutano wa viongozi na wafadhili wa kimataifa kusaka euro bilioni 7.5 kwa ajili ya kuimarisha nguvu za kutafuta, kutengeneza na kusambaza chanjo dhidi ya janga la maradhi ya COVID-19.

https://p.dw.com/p/3blIr
Europäisches Parlament Ursula von der Leyen
Picha: Getty Images/AP/K. Tribouillard

Zaidi ya nusu ya vifo vya COVID-19 vimetokea barani Ulaya, bara ambalo limeripoti hadi sasa kupoteza watu 140,000. Mwenyeji wa mkutano huo wa wafadhili uliofanyika kwa njia ya mtandao, Rais wa Kamisheni ya Ulaya Ursula von der Leyen, amesema kuwa chanjo ndiyo njia bora zaidi ya kulikabili janga hili. 

Kamisheni hiyo kwa upande wake imeahidi kutoa euro bilioni moja, huku von der Leyen akisema huo ni mchango wa kile alichokiita Timu ya Ulaya, huku Rais wa Baraza la Ulaya, Charles Michel, akiziita siku za sasa kuwa za giza, lakini zilizo muhimu kwa kuwa zinabainisha ubinaadamu wetu.

Ufaransa kwa upande wake imechangia euro milioni 500 katika mpango huo wa kusaka chanjo dhidi ya virusi vya korona uliopewa jina la ACT-A, kwa mujibu wa Rais Emmanuel Macron. 

Waziri Mkuu wa Uhispania, Pedro Sanchez, ambaye nchi yake ina idadi kubwa ya maambukizo ya corona, ameahidi kutoa euro milioni 125, ambapo milioni 50 zitakwenda kwenye mpango wa kutafuta chanjo na milioni 75 kwenye kile kinachoitwa Muungano wa Utayarifu kwenye Uchunguzi wa Maradhi Yanayoambukiza.

Kando ya Ufaransa na Uhispania, mataifa mengine yaliyotazamiwa kuahidi kiwango kikubwa cha fedha ni Ujerumani, Uingereza na Italia. 

Waziri Mkuu wa Japan Shinzo Abe kwa upande wake alitarajiwa kutowa ahadi ya kuchangia, lakini msimamo wa China, ambako ndiko mripuko wa maradhi hayo ulikoanzia, haukufahamika mara moja licha ya kuwakilishwa na balozi wake kwenye Umoja wa Ulaya.

Marekani haishiriki

USA Coronavirus Donald Trump
Rais Donald Trump wa Marekani ambaye nchi yake haikushiriki mkutano wa kimataifa kukusanya fedha kwa ajili ya kupambana na janga la COVID-19.Picha: Reuters/C. Barria

Kwa ujumla, mataifa 40, pamoja na Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada, ukiwemo Wakfu wa Bill na Melinda Gates, na taasisi za utafiti ni sehemu ya mkutano huu wa harambee.

Lakini, wakati mataifa yenye nguvu barani Ulaya yakijipanga kutoa ahadi zao za ufadhili kwenye mkutano huo, kutokuhudhuria kwa Marekani kunatajwa kudhoofisha uwezekano wa kuwa na juhudi za pamoja za kuendeleza na kuzalisha chanjo inayohitajika.

Hata hivyo, msemaji wa ubalozi wa Marekani kwenye ofisi za Umoja wa Mataifa mjini Geneva, amesema kuwa serikali ya Trump inaunga mkono jitihada za mataifa mengine kusaka fedha za kutafiti na hatimaye kulitokomeza janga la COVID-19 kama ulivyo mkutano wa leo wa wafadhili.

Hapo jana, Trump, ambaye anawania kuchaguliwa tena kwa uchaguzi wa Novemba, alisema Marekani itakuwa tayari imegunduwa chanjo kufikia mwishoni mwa mwaka huu. Hata hivyo, utabiri huo unatiliwa mashaka na wengine, huku Waziri wa Afya wa Ujerumani Jens Spahn akionya kwamba inaweza kuchukuwa miaka kadhaa kupatikana. 

Afisa mmoja wa Umoja wa Ulaya ameliambia shirika la habari licha ya Umoja huo kuitikia wito wa kuwa na hatua ya pamoja kilimwengu kulikabili janga hili, ni serikali ya Marekani ndiyo inayojitenga yenyewe, lakini wanafanya kazi kwa karibu na taasisi binafsi za Marekani, kama vile Wakfu wa Bill na Melinda Gates, ambazo zina fedha na ushawishi mkubwa.

AFP/Reuters