1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Ulaya watoa yuro Bilioni moja kuisaidia Afghanistan

12 Oktoba 2021

Fedha za Umoja wa Ulaya zitapelekwa moja kwa moja kwa wananchi na sio kwa serikali ya Taliban ambayo haitambuliwi na Umoja huo

https://p.dw.com/p/41aJF
Brüssel | Sondertreffen der EU-Außenminister | Konflikt in Afghanistan
Picha: Johanna GeronReuters/AP/dpa/picture alliance

Viongozi wa nchi tajiri kiviwanda na zile zinazoinukia kiuchumi  wa kundi la G20 wamekutana leo kwenye mkutano maalum wa kilele unaofanyika kwa njia ya mtandao,kujadili mgogoro wa kibinaadamu unaojitokeza huko Afghanistan. Saumu Mwasimba anafuatilia mkutano na hii hapa taarifa yake.

 Umoja wa Ulaya umeufungua mkutano huo kwa kutangaza msaada wa yuro bilioni moja kwa Afghanistan. Rais wa Marekani Joe Biden na waziri mkuu wa India Narendra Modi ni miongoni mwa walioshiriki mkutano huo unaoongozwa na Italia ingawa rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa Urusi Vladmir Putin waliwatuma wawakilishi wao.

Wakati mkutano huo ulipofunguliwa mkuu wa halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen alitangaza msaada unaotolewa na jumuiya hiyo kwa ajili ya kuepusha janga kubwa la kibinadamu na matatizo ya kijamii na kiuchumi nchini Afghanistan. Fedha zilizotolewa na Umoja huo zinajumuisha yuro milioni 250 kwenye jumla ya yuro milioni 300 ambazo awali zilitolewa na Umoja huo kwa ajili ya kusimamia mahitaji ya dharura ya kibinadamu huku nyingine zilizobakia zikipelekwa kwa nchi jirani na Afghanistan ambazo zimekuwa zikiwakaribisha raia wa Afghanistan wanaowakimbia Taliban.

Gymnich-Treffen in Brdo Slowenien
Picha: Florian Gaertner/photothek/picture alliance

Taarifa ya Umoja wa Ulaya imekumbusha kwa kutoa msisitizo kwamba fedha zake zinakusudiwa kuwafikia moja kwa moja waafghanistan na kuwapa msaada wa moja kwa moja na zitafikishwa kupitia mashirika ya kimataifa yanayofanya kazi ndani ya Afghanistan na wala hazitokwenda kwa serikali ya mpito ya Taliban ambayo Umoja wa huo wa Ulaya mjini Brussels hauitambui.Ikumbukwe kwamba msaada wa maelendeleo unaotolewa na Umoja wa Ulaya ni tofauti na msaada wa kibinadamu na msaada huo bado umesitishwa.

Lakini pia ni mkutano unaofanyika katika wakati ambapo kundi la Taliban limefanya mazungumzo yake ya kwanza ya ana kwa ana na wajumbe kutoka Umoja wa Ulöaya na Marekani,mkutano uliofanyika huko Doha nchini Qatar ambapo kundi hilo linaendeleza juhudi za kidiplomasia likilenga kutafuta uungwaji mkono wa kimataifa. Na kwenye mkutano huo wa Qatar kaimu waziri wa mambo ya nje wa serikali ya Taliban Amir Khan Muttaqi alikuwa na salamu za wazi kwa Umoja wa Ulaya.

Afghanistan Taliban-Vertreter führen in Doha Gespräche mit US-amerikanischen und europäischen Delegierten
Picha: Stringer/REUTERS

"Ingelikuwa hakuna chochote kizuri kuhusu Afghanistan,nyote hamudhani kwamba kungeonekana kundi kubwa kabisa la wanaokimbilia Ulaya? Ulaya inapata faida gani?hakuna.Kwa wale wanaoratibu kuwasafirisha waafghanistan ulaya,tunawaomba badala ya kupoteza rasilimali kumshughulia mtu mmoja,badilisheni maisha ya watu 10 walioko ndani ya Afghanistan kwa kutumia rasilimali hizohizo. Afghanistan ni nchi ya rotuba,ina maji mazuri,ina rasilimali asili,ina madini na sasa ina serikali yenye uwezo.

Msaada wa kimataifa kuelekea Afghanistan umesitishwa tangu kundi la Taliban liliporudi tena madarakani baada ya jeshi la Marekani na vikosi vingine vya kimataifa kuondoka baada ya miaka 20 ya vita katika taifa hilo. Mali za nchi hiyo zilizoko nje zimezuiwa wakati bei ya vyakula na ukosefu wa ajira vikipanda hali ambayo inaongeza wasiwasi wa kushuhudiwa janga kubwa la kibinadamu pale msimu wa baridi kali utakapoingia.

 

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW