Umwagaji damu wafikia kilele kipya Syria
16 Novemba 2011Hayo ni kwa mujibu wa makundi ya haki za binadamu na wanaharakati walio uhamishoni. Wengi wa wahanga wa umwagaji damu uliotokea siku ya Jumatatu, walikuwa wanajeshi, ikidaiwa kuwa walishambuliwa na wanajeshi walioasi. Mapigano ya mara kwa mara, kati ya wanajeshi na wale walioasi yanaripotiwa kutoka mikoa ya Deraa na Idlib.
Kwa mujibu wa matamshi ya Waziri Mkuu wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, nchi yake imepoteza imani katika serikali ya Syria. Akizungumza mjini Ankara, Erdogan amesema, vitendo vya ukatili vya Assad vinamhatarisha kuingia katika orodha ya viongozi wa kisiasa wanaotawala kwa mabavu. Uturuki inashinikiza kuiwekea Syria vikwazo ambavyo havitouathiri umma wa nchi hiyo. Wakati huo huo, wajumbe wa upinzani wa baraza la taifa la Syria waliokuwa ziarani Moscow, hawakufanikiwa kuishawishi serikali ya Urusi kuchukua hatua kali dhidi ya Assad.