UN: Ukiukaji wa haki za binadamu unaendelea Burundi
5 Septemba 2018Katika ripoti yake ya kwanza ya mwaka jana, Tume ya uchunguzi ya Umoja wa Mataifa kuhusu Burundi ilisema kuna ushahidi wa kutosha kuamini kuwa serikali ya Burundi inahusika katika uhalifu dhidi ya binadamu.
Hii leo, tume hiyo imesema uhalifu huo bado unaendelea, ikitaja mauaji ya kiholela, watu kulazimika kupotea, kuzuiwa kwa watu bila ya kufunguliwa mashitaka, mateso na udhalilishaji wa kingono.
Ripoti hiyo mpya ya Umoja wa Mataifa imeendelea kusema matukio ya kutisha ya ukiukaji wa haki za binadamu, yakiwemo yale yanayoweza kutajwa kuwa uhalifu dhidi ya binadamu yanaendelea kushuhudiwa Burundi kuanzia mwaka jana hadi mwaka huu.
Jeshi na Polisi zatuhumiwa
Taarifa kutoka mkuu wa tume hiyo ya wachunguzi Doudou Diene imesema kutupwa kwa miili au maovu kufanywa usiku, yanapelekea matukio hayo kutoonekana wazi wazi, lakini licha ya hayo, bado yanarekodiwa kufanyika.
Burundi ilitumbika katika mzozo wa kisiasa mwaka 2015 baada ya Rais Nkurunziza kutangaza anagombea muhula wa tatu madarakani kinyume na katiba.
Mzozo huo umesababisha mauaji ya takriban watu 1,200 na kuwalazimu wengine laki nne kuyahama makazi yao, hali iliyosababisha mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya binadamu ICC kuanzisha uchunguzi.
Wachunguzi wa Umoja wa Mataifa wamesema wana orodha ya wanaodaiwa kufanya uhalifu dhidi ya binadamu na wataiwasilisha orodha hiyo kwa asasi yoyote itakayotwishwa wajibu wa kuendesha uchunguzi huru na wa kuaminika kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu nchini Burundi na ambayo itatoa hakikisho la kuwapa ulinzi mashahidi.
Matamshi ya Rais yasababisha chuki na maovu
Diene amesisitiza kuwa idara ya mahakama ya Burundi haina ari wala uwezo wa kung'amua au kuwashitaki wanaohusika na maovu yanayojiri nchini humo na kuongeza kuwa mahakama imekuwa ikitumika kama chombo cha ukandamizaji kinachotumika na muhimili wa rais kuzima maandamano yoyote na upinzani.
Mazingira ya kukiuka haki na kutojali sheria yameendelea ikiwemo chuki na ghasia zinazoendekezwa na viongozi akiwemo Rais na wanachama wa chama tawala CNDD-FDD.
Tume hiyo haikutaja majina ya washukiwa lakini imesema maafisa wa shirika la kitaifa la ujasusi, polisi, wanajeshi na wanachama wa tawi la vijana la chama tawala lijulikanalo Imbonerakure ndiyo waliohusika katika maovu mabaya dhidi ya binadamu.
Umoja wa Mataifa umesema Imbonerakure imezidi kuwa na nguvu huku nafasi ya demokrasia nchini humo ikizidi kupungua.
Ripoti hiyo ya wachunguzi inatarajiwa kuwasilishwa kwa baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu haki za binadamu baadaye mwezi huu, na wameliomba baraza hilo kurefusha muda wao wa kuhudumu kwani kuna umuhimu wa kuendelea na majukumu yao wakati Burundi ikijitayarisha kwa uchaguzi mpya mwaka 2020, ambao tayari unashuhudia ukiukaji wa haki za binadamu.
Utawala wa Burundi umejaribu na kufeli kuizuia tume hiyo ya wachunguzi iliyoundwa mwaka 2016 kuendesha uchunguzi na matokeo yake imekataa kutoa ushirikiano.
Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman