1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaRwanda

UN: Vikosi vya Rwanda vyasaidiana na M23 kupigana Kongo

8 Julai 2024

Ripoti moja ya wataalam wa Umoja wa Mataifa iliyoonekana na shirika la habari la Ufaransa AFP inasema, kati ya wanajeshi 3000 hadi 4000 wa Rwanda wanashirikiana na waasi wa M23 katika mapigano mashariki mwa Kongo.

https://p.dw.com/p/4i0Va
Kigali, Rwanda | Wanajeshi wa Rwanda wakiwa njiani kuelekea Msumbiji
Wanajeshi wa Rwanda RDFPicha: Cyril Ndegeya/Xinhua/picture alliance

Ripoti hiyo inasema Kigali, ndiyo inayodhibiti operesheni za waasi hao wa M23.

Watafiti wa ripoti hiyo walikadiria wakati wa kuandikwa kwake mnamo mwezi Aprili kwamba, idadi ya vikosi vya Rwanda inalingana au imeivuka idadi ya waasi wa M23 ambayo ilikuwa inadaiwa kuwa karibu 3,000.

Ripoti hiyo inajumuisha picha zilizohakikiwa, mikanda ya video, picha zilizopigwa na droni, ushuhuda na ripoti za majasusi mambo yanayothibitisha uingiaji wa jeshi la Rwanda RDF huko mashariki mwa Kongo.

Kigali, Ruanda | Wanajeshi wa Rwanda wakiwa njiani kuelekea Msumbiji
Wanajeshi wa Rwanda RDFPicha: Simon Wohlfahrt/AFP

Watoto kusajiliwa jeshini

Mikanda hiyo ya video na picha zinaonesha milolongo ya wanajeshiwaliojihami wakitumia silaha na magari ya kijeshi yaliyo na mifumo ya kuzuia mashambulizi ya makombora ya ndege. Picha hizo pia zinaonesha malori yanayotumiwa kuwasafirisha wanajeshi.

Vile vile ripoti hiyo inaeleza kwamba watoto kuanzia umri wa miaka 12 wamesajiliwa kutoka walau kila kambi ya wakimbizi ndani ya Rwanda na wanapelekwa katika kambi za mazoezi katika maeneo ya waasi chini ya usimamizi wa wanajeshi wa Rwanda na wanamgambo wa M23.

Inaongeza kwamba watoto walio na umri wa miaka 15 na zaidi wanapewa mafunzo ya kijeshi na kupelekwa vitani ili kuwa katika mstari wa mbele kushiriki mapigano hayo.

Wataalam hao wa Umoja wa Mataifa wanadai kwamba kusajiliwa kwa watoto jeshini nchini Rwanda, ni jambo linalofanywa na maafisa wa ujasusi wakitoa ahadi za uongo za mishahara na malipo kwa watoto hao. Inaripotiwa kwamba wale wanaopinga, wanachukuliwa na kusajiliwa jeshini kwa nguvu.

Rwanda iliwasaidia waasi kunyakua maeneo mengi zaidi

Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo imekuwa ikiituhumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23 ila Kigali imekuwa mara zote ikikanusha vikali tuhuma hizo.

DR Kongo Kibumba 2022 | Waasi wa M23
Waasi wa M23 Picha: Moses Sawasawa/AP Photo/picture alliance

Lakini ripoti hiyo iliyoitishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, inasema hatua ya jeshi la Rwanda kuzidhibiti harakati za waasi wa M23 ni jambo linaloifanya nchi hiyo kulaumiwa kwa vitendo vya waasi hao.

Kulingana na wataalam hao wa Umoja wa Mataifa, uingiliaji wa jeshi la Rwanda na operesheni zake za kijeshi katika mkoa wa Kivu Kaskazini katika maeneo ya Nyiragongo, Rutshuru na Masisi, ulikuwa muhimu kwa waasi hao kutanua maeneo zaidi inayoyadhibiti kati ya Januari na Machi mwaka huu.

Mkoa wa Kivu Kaskazini umekuwa chini ya udhibiti wa waasi wa M23 tangu mwishoni mwa mwaka 2021, huku kundi hilo likinyakua maeneo makubwa na kuanzisha utawala wa kivyake katika maeneo ambayo sasa yako chini ya udhibiti wake.

Chanzo: AFP