UN: Waafghanistan wasilazimishwe kurudi nchini mwao
17 Agosti 2021Shirika la kushughulikia wakimbizi la UNHCR limezishauri nchi kutowarudisha kwao raia wa Afghanistan, wakiwemo raia wa taifa hilo ambao maombi yao ya kutaka hifadhi yamekataliwa.
Msemaji wa UNHCR Shabia Mantoo amewaambia waandishi habari mjini Geneva kuwa, kufuatia kudodora kwa usalama na mzozo mbaya wa kibinadamu nchini Afghanistan, UNHCR imeyahimiza mataifa kusimamisha mipango ya kuwarudisha makwao raia wa Afghanistan.
Mantoo amekaribisha hatua ya baadhi ya mataifa ya Ulaya yaliyosimamisha mpango wa kuwarudisha kwa nguvu raia wa Afghanistan, na kuonyesha matumaini kuwa mataifa mengine pia yataiga.
Msemaji huyo wa UNHCR amesema hata kabla ya kuanza kwa machafuko ya hivi karibuni, zaidi ya Waafghani 550,000 wamepoteza makaazi yao kutokana na mizozo na ukosefu wa usalama kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu.