UN: Wanawake ni waathirika wakuu wa biashara ya binaadamu
7 Januari 2019Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2018 kuhusu biashara ya binaadamu ulimwenguni iliyotolewa leo na ofisi hiyo ya UNODC, wafanyabiashara hao ulimwenguni wameendelea kuwalenga wanawake na wasichana. Mkuu wa ofisi ya UNODC, Yury Fedotov amesema katika ripoti hiyo kwamba karibu robo tatu ya waathirika waligundulika walikuwa kwa ajili ya kutumikishwa kingono na asilimia 35 ya hao waliosafirishwa na kulazimishwa kufanya kazi, ni wanawake.
Ripoti hiyo imeeleza kuwa vita, utawala mbovu wa sheria na hali mbaya ya kiuchumi na kijamii katika baadhi ya mataifa ya Mashariki ya Kati, Afrika na Asia ndiyo mambo yaliyochangia kwa kiasi kikubwa biashara hiyo haramu, ambayo husababisha utumwa wa ngono, unyanyasaji wa kijinsia na ndoa za lazima.
Aidha, idadi ya watu waliolazimika kuyakimbia makaazi yao kutokana na vita na mateso katika nchi za Syria, Iraq, Afghanistan na Myanmar ndiyo wamekuwa wakilengwa na wafanyabiashara hao haramu, kama wanavyowalenga wahamiaji na wakimbizi wanaosafiri kupitia maeneo yenye mizozo kama vile Libya au maeneo ya kusini mwa Jangwa la Sahara.
Ripoti hiyo imebainisha kuwa nchi tajiri za Ulaya, Amerika ya Kaskazini na Mashariki ya Kati zimeendelea kuwa maeneo ambako wanapelekwa waathirika wa biashara ya binaadamu. Wengi wa waliogundulika kutumikishwa kingono, walikuwa katika maeneo ya nchi hizo.
UNODC inazitolea mfano nchi za Magharibi na Kusini mwa Ulaya kwamba watu wengi waliosafirishwa walikuwa ni kwa ajili ya kufanya kazi au unyanyasaji wa kingono, huku asilimia 25 wakiwa waathirika wanaotoka katika ukanda huo na asilimia 33 wakitokea Ulaya ya kati pamoja na kusini mashariki mwa bara hilo.
Idadi yaongezeka
Idadi ya visa vya biashara ya binaadamu pia imeongezeka ulimwenguni kote. Mwaka 2016 visa 25,000 kuhusu aina zote za biashara ya binaadamu viliripotiwa, ongezeko la asilimia 40 zaidi ikilinganishwa na mwaka 2011, ambapo kulikuwa na visa 10,000.
Hata hivyo, Umoja wa Mataifa umeonya kuwa ongezeko hilo huenda limechangiwa na kugunduliwa kwa waathirika, kuliko kuongezeka kwa namba ya watu wanaosafirishwa. Ripoti hiyo imebaini kuwa wengi wa waathirika wanagunduliwa katika nchi zao za kuzaliwa.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, visa 100 vya kuondolewa kwa viungo vya mwili viliripotiwa pia katika kipindi cha mwaka 2014 hadi 2017, hasa katika Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/ AFP, DW https://bit.ly/2QthyTi
Mhariri: Josephat Charo