UN yaitaka Israel iondoe marufuku ya misaada Gaza
26 Machi 2024Shirika la Umoja wa Mataifa linalowashughulikia Wakimbizi wa Palestina UNRWA ndilo lililokuwa na jukumu hilo. Umoja wa Mataifa unadai watu katika eneo hilo wanakufa vifo vya kinyama kutokana na njaa. Hapo jana Israel ilisema haitofanya kazi tena na UNRWA ikidai shirika hilo linauchochea mzozo huo.
UNRWA imekuwa katika mzozo tangu Israel iwatuhumu baadhi ya wafanyakazi wake kwa kuhusika katika uvamizi wa Hamas wa Oktoba 7 dhidi ya Israel.
Shirika hilo liliwaachisha baadhi ya wafanyakazi wake kutokana na tuhuma hizo na madai hayo yanachunguzwa. Hayo yakiarifiwa, Qatar ambaye ndiye mpatanishi mkuu katika mazungumzo ya kusitisha vita na kuachiwa kwa mateka imesema, mazungumzo bado yanaendelea, licha ya pande zinazozozana kulaumiana kutokana na kukosekana kwa suluhu kwenye mazungumzo hayo.