1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yataka kukagua kinu cha nyuklia cha Ukraine

Sylvia Mwehozi
4 Agosti 2022

Shirika la Umoja wa Mataifa linalofuatilia masuala ya nyuklia, limetoa wito wa kukifikia kinu cha nyuklia cha Ukraine ambacho sasa kinadhibitiwa na vikosi vya Urusi, ili kubaini kama ni chanzo cha hatari.

https://p.dw.com/p/4F785
Ukraine Kernkraftwerk Saporischschja
Picha: Dmytro Smolyenko/imago images

Mkuu wa shirika la kimataifa la kudhibiti silaha za nyuklia, IAEA Rafael Grossi ameliambia gazeti moja la Uswisi la Tages-Anzeiger kwamba kinu kikubwa cha nyuklia barani Ulaya ambacho kipo eneo la Zaporizhzhia na kuendeshwa na mafundi wa Ukraine, kwa hivi sasa kipo katika hali "tete" na mawasiliano hayafanyi kazi kila siku. Grossi ameongeza kuwa wanafahamu kumekuwa na madai ya kuhifadhiwa risasi na mashambulizi dhidi ya kinu hicho.Umoja wa Ulaya waomba usalama wa nyuklia kuangaziwa

"Ili kituo chochote cha nyuklia kifanye kazi kwa kawaida na kwa usalama, kuna kanuni kadhaa ambazo lazima zizingatiwe. Na tunapoangalia hali ya kipekee tuliyonayo huko Zaporizhzhya, tunaona kwamba kanuni nyingi, kama si zote, zinakiukwa au kutozingatiwa na kufuatwa," alisema Grossi.

Afisa mmoja wa Urusi nchini Ukraine alisema Jumatano kwamba vikosi vya Ukraine mara kwa mara vimetumia silaha za Magharibi kushambulia kinu hicho ambacho kina mitambo miwili kati ya sita inayofanya kazi na kimekuwa kitovu cha tahadhari za mara kwa mara kutoka Ukraine, nchi za Magharibi na Urusi.

Libanon - syrisches Frachtschiff Laodicea in Tripolis
Meli ya Syria inayodaiwa kubeba nafaka zilizoibiwa UkrainePicha: picture alliance/AP

Huku hayo yakijiri, Ukraine imedai kwamba Urusi imeanza kuunda kikosi cha kijeshi kinachoulenga mji aliozaliwa rais Volodmyr Zelensky wa Kryvyi Rih wakati Jumuiya ya kujihami ya NATO ikikaribia kujipanua zaidi ndani ya miongo kadhaa.

Bunge la seneti la Marekani na lile la Italia siku ya Jumatano ziliidhinisha kujiunga kwa Finland na Sweden ndani ya muungano huo wa kijeshi wenye wanachama 30. Chini ya uanachama wa NATO ambao ni lazima uridhiwe na wanachama wote 30, shambulio dhidi ya mwanachama mmoja ni shambulio dhidi ya wanachama wote.Hatimaye Meli yenye nafaka yaelekea Lebanon

Rais wa Marekani Joe Biden amesema "kura hiyo ya kihistoria inatoa ishara muhimu ya dhamira endelevu, ya vyama vyote vya Marekani kwa NATO", na kuhakikisha kwamba muungano huo unajiandaa kwa changamoto yoyote ya sasa na baadae. Urusi ambayo iliivamia Ukraine mnamo Februari 24 mara kwa mara imeonya juu ya Finland na Sweden kujiunga NATO.

Na meli ya Syria ambayo Ukraine inadai kuwa imebeba nafaka zilizoibwa kutoka Ukraine imeruhisiwa kuondoka katika bandari ya Lebanon baada ya maafisa kuipa idhini kufuatia ukaguzi. Meli hiyo ya Laodicea ilitia nanga katika bandari ya Tripoli tangu ilipoawasili Alhamisi iliyopita, ikiwa na jumla ya tani 10,000 za nafaka na shayiri. Ukraine inadai kwamba nafaka hizo ziliibwa na Urusi madai ambayo Moscow inayakanusha.