UN yawawekea vikwazo waasi wa Kongo
21 Februari 2024Kamati ya Baraza la Usalama inayoshughulikia vikwazo vya Kongo imetangaza vikwazo vya silaha, marufuku ya kusafiri na kuzuiliwa mali za viongozi wawili wa kundi la ADF, mmoja kutoka kundi la Twirwaneho na mmoja kutoka kundi la waasi la Muungano wa Kitaifa kwa Uhuru wa Kongo - CNPSC. Aidha walioongezwa kwenye orodha hiyo ya Umoja wa Mataifa ni msemaji wa kijeshi wa waasi wa M23 na kiongozi mmoja wa waasi wa FDLR.
Akizungunza katika mkutano wa dharura wa Umoja wa Mataifa mjini New York, naibu balozi wa Marekani Robert Wood amezionya Rwanda na Kongo kuwa lazima zirudi nyuma kutoka ukingo wa vita.
Wood amesema pande zinazohusika na mgogoro huo na washiriki wa kikanda wanapaswa kuendelea maramoja na michakato ya amani ya mjini Nairobi na Rwanda – juhudi za kidiplomasia, sio mgogoro wa kijeshi, ndio njia pekee ya suluhisho litakalopatikana kwenye mazungumzo hayo na kuleta amani endelevu.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaungwa mkono na makundi kadhaa yenye silaha, kampuni mbili za kigeni na uwepo wa wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa ma askari kutoka Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika – SADC.
Amnesty yahimiza kusitishwa mashambulizi
Nalo shirika la Kimataifa la Haki za Binaadamu Amnesty International limetoa wito wa kusitishwa mara moja kwa kile ilichoelezea kuwa ni mashambulizi ya makusudi na ya kiholela dhidi ya raia, katika mapigano kati ya vikosi vya serikali na waasi wa M23 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Mkurugenzi mkuu wa Amnesty kanda ya mashariki na kusini mwa Afrika Tigere Chagutah amesema makabiliano hayo yamesababisha vifo vya raia 35 na mamia kujeruhiwa. Amesema maelfu ya raia kwa mara nyingine wamenasa katika mapigano hayo na wanahitaji msaada wa dharura wa kiutu.
Ameongeza kuwa zaidi ya watu milioni moja sasa wako ndani na karibu ya mji wa Goma baada ya kukimbia mapigano. Kongo, Umoja wa Mataifa na nchi za Magharibi zinasema Rwanda inawaunga mkono waasi katika jaribio la kudhibiti raslimali kubwa za madini, madai ambayo Kigali inakanusha. Baada ya miezi kadhaa ya utulivu, mapigano makali yalizuka mwezi uliopita karibu na Goma, mji mkuu wa mkoa wa Kivu Kaskazini.
Waziri Mkuu Lukonde ajiuzulu
Waziri mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo Jean-Michel Sama Lukonde amejiuzulu, hatua inayosababisha kuvunjwa serikali yake. Waziri mkuu huyo aliwasilisha barua yake ya kujiuzulu kwa Rais Felix Tshisekedi siku nane baada ya kuidhinishwa kwa nafasi yake kama mbunge wa kitaifa. Sasa atahudumu bungeni katika nafasi ya ubunge.
Ofisi ya rais imesema ombi lake la kujiuzulu limekubaliwa. Hata hivyo, rais ameiomba serikali ya Lukonde kuendelea kuyashughulikia masuala ya sasa hadi pale serikali mpya itakapoundwa. Haikutoa sababu za kujiuzulu kwa waziri mkuu.
Lukonde aliteuliwa waziri mkuu wa nchi hiyo yenye utajiri wa madini Februari 2021. Alikuwa na umri wa miaka 43 wakati huo.
AFP, Reuters