1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN: Zaidi ya raia 1,300 wameuawa katika machafuko, DRC

31 Machi 2023

Shirika la Haki za Binaadamu la Umoja wa Mataifa limelani vikali kuongezeka kwa machafuko katika eneo la mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, sambamba na visa vingi vya unyanyasaji wa kingono.

https://p.dw.com/p/4PXVG
Schweiz, Genf: Volker Türk, UN-Hochkommissar für Menschenrechte
Picha: Salvatore Di Nolfi/KEYSTONE/dpa/picture alliance

Kamishna mkuu wa shirika hilo la Umoja wa Mataifa la haki za binaadamu Volker Turk ameonya mbele ya Baraza la shirika hilo kuhusu makundi ya waasi yaliyolizunguka eneo hilo kwa miongo kadhaa ambao wanaimarisha mashambulizi dhidi ya raia hasa huko Ituri na Kivu ya Kaskazini.

Amesema makundi ya wanamgambo ya CODECO, M23 na mengineyo yameendelea kufanya mashambulizi yasiyoelezeka dhidi ya raia na kuongeza kuwa tangu Oktoba mwaka 2022, karibu watu 1,334 ambao ni pamoja na watoto 107 wameuawa katika majimbo ya mashariki. Mbali na waliouawa, karibu raia milioni sita nchini humo wameyakimbia makazi yao, idadi ambayo ni kubwa zaidi ya wakimbizi wa ndani barani Afrika.

Soma Zaidi: Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wawasili DRC

Kulingana na Turk, mashaka yaliyopo sasa ni kwamba machafuko hayo yanaingia kwenye maeneo ambayo hayakuwahi kuguswa ikiwa ni pamoja na majimbo ya Mai-Ndombe na Kwilu, kaskazini mwa nchi hiyo, ambayo tayari yameanza kushuhudia mashambulizi ya hapa na pale. Ametoa mfano wa mashambulizi ya Ijumaa iliyopita katika jimbo la Kwilu ambako watu 14 waliuliwa, miongoni mwao walikatwakatwa kwa mapanga, hii ikiwa ni kulingana na afisa mmoja wa eneo hilo.

Kongo I Kanyaruchinya Lager für Binnenvertriebene
Maelfu ya raia wameyakimbia makazi yao mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kutokana na mashambulizi ya M23.Picha: Guerchom Ndebo/AFP

Turko aelezea hofu ya kuongezeka kwa mvutano kati ya Rwanda na DRC.

Aidha, Turk amekosoa kuongezeka kwa mvutano kati ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Rwanda ambapo ameonya hali hiyo inachochea kuongezeka kwa matamshi ya chuki. Kinshasa na baadhi ya mataifa ya Magharibi wanasema waasi wa M23 wanaungwa mkono na Rwanda inayoyatamani madini yaliyotapakaa kote katika eneo la mpaka, madai ambayo Kigali inakataa kata kata.

Mwaka 2022 tu, Umoja wa Mataifa ulirekodi na kuthibitisha visa 701 vinavyohusiana na unyanyasaji wa kingono katikati ya mzozo, vilivyohusisha wanawake 503, wanaume 11 na wasichana 187, ambavyo kwa kiasi kikubwa vilitokana na utovu wa nidhamu na ufisadi.

Hata hivyo, amezisifu mamlaka kwa kuchukua hatua madhubuti katika kukabiliana na utovu wa nidhamu, na kuwaadhibu takribani wanajeshi 91 wa vikosi vya ulinzi na usalama na wengine 143 wa makundi ya wanamgambo wanaokabiliwa na tuhuma zinazohusiana na ukiukaji wa haki walivyovofanya mwaka uliopita.

Soma Zaidi:Umoja wa Mataifa wataja "kushtushwa" na mauaji mashariki mwa Kongo