1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UNICEF: Watoto milioni 11 wanategemea misaada Yemen

Angela Mdungu
24 Machi 2023

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhuduma watoto duniani UNICEF limesema, takribani watoto milioni 11 wanategemea misaada ya kiutu katika taifa la Yemen.

https://p.dw.com/p/4PAn2
Jemen | Unterernährtes Kind
Picha: Mohammed Mohammed/Photoshot/picture alliance

Shirika hilo limetahadharisha kuwa karibu wasichana na wavulana milioni 2.2 nchini humo wana utapiamlo na kwamba bila ya hatua za haraka za kukabiliana na hali hiyo, huenda hatari ikawa kubwa zaidi.

Shirika la Umoja wa mataifa la kuhudumia watoto duniani katika taarifa yake iliyotolewa mapema leo imeongeza kuwa zaidi ya watoto 540,000 nchini Yemen wameathiriwa vibaya zaidi na utapiamlo kiasi kwamba maisha yao yako hatarini ikiwa hawatopata matibabu ya haraka. Nchi hiyo, imekuwa katika vita vya wenyewe kwa wenyewe kwa miaka mingi. Vita hivyo vinahusisha muungano wa kijeshi unaoongozwa na Saudia dhidi ya waasi wa Kihouthi wanaoungwa mkono na Iran.

Soma zaidi: UNICEF: Watoto 1,000 wanakufa kila siku kwa kunywa maji machafu

Pande hizo mbili zimekuwa zikipambana tangu mwaka 2014 wakati waasi wa Kihouthi walipofanikiwa kuuteka mji mkuu Sana'a na miji mingine miwili hali iliyoifanya serikali kukimbilia upande wa Kusini. Mnamo mwezi Machi mwaka 2015, Saudi Arabia ilianzisha muungano wa kijeshi unaounga mkono wanajeshi wa serikali wakati wa Houthi walipoanza kusonga mbele kuelekea mji wa Aden ambako serikali imeweka makao yake kwa muda.

Watoto wakicheza mbele ya magari yaliyoharibiwa kwa mabomu huko Taizz, Yemen
Watoto wakicheza mbele ya magari yaliyoharibiwa kwa mabomu huko Taizz, YemenPicha: Abdulnasser Alseddik/AA/picture alliance

Kwa mujibu wa taarifa hiyo shirika la kuhudumia watoto duniani, miaka minane ya ya vita vya wenyewe kwa wenyewe imesababisha anguko la uchumi hali iliyoathiri usambazaji wa huduma muhimu kwa raia jambo lililochochea kuibuka kwa mgogoro mkubwa wa kiutu nchini Yemen. Ripoti hiyo inasema zaidi ya watoto 110,000 waliuwawa au walijeruhiwa vibaya kati ya mwaka 2015 na 2022.

Ustawi wa watoto hatarini

Ustawi wa watoto nchini humo unatishiwa zaidi na maamuzi yaliyofanywa na familia zao zenye dhiki. Maamuzi hayo ni kama vile ndoa za utotoni, ajira kwa watoto au kuajiriwa jeshini. Shirika hilo la kuhudumia watoto duniani limeeleza kuwa linahitaji kiasi cha dola milioni 484 mwaka huu ili kuendelea kutoa msaada kwa watoto nchini humo na kuchukua hatua muhimu kuhakikisha mahitaji muhimu na ustawi wa watoto.

UNICEF limetahadharisha kuwa ikiwa halitaongezewa ufadhili, huenda likalazimika kupunguza misaada kwa watoto wanaoishi katika mazingira magumu katika taifa hilo la Yemen lilioathiriwa vibaya na vita.Taarifa ya shirika hilo imeongeza kuwa, zaidi ya watu milioni 21.7 ambayo ni theluthi mbili ya idadi ya watu nchini humo wanahitaji msaada wa kiutu mwaka huu.

Chanzo:DPAE/AFPE