Uongozi mpya katika chama cha kiliberali cha FDP
5 Aprili 2011Tuanzie lakini na eti eti zilizohanikiza kuhusu nani atachaguliwa kuwa mwenyekiti wa chama cha FDP.Gazeti la "Stuttgarter Nachrichten" linahisi:
"Suala sio nani atapanda darajani.Rösler au mwengine.Muhimu zaidi ni kama viongozi wepya watalingana,kuanzia wazee waliobobea akina Gerhardt na Solms na kufikia wepya ambao hawajazoweya mawimbi hatari baharini akina Lindner na Bahr.Bila ya kuwataja wale ambao hata mawimbi madogo yanaweza kuwapindua akina Homburger,Brüderle na Pieper.FDP wanataka kurejea uwanjani.Kwa hivyo itakuwa vyema .mbali na nahodha,wakijipatia na dira pia.
Kuna la ziada pia wana FDP wanalolihitaji,linaandika gazeti la "Westdeutsche Zeitung" la mjini Düsseldorf:
"Kwanza lazma mjadala ufanyike kuhusu muongozo ,baadae ndipo watu watakapoweza kuzungumzia nani akabidhiwe nini na majukumu yepi.Katika utaratibu huo ndipo FPD itakapoweza kugundua kwamba sio tuu vijana wanastahiki kuongoza mustakba wao bali katika maisha ya kisiasa wenye maarifa wanasaidia sana kurejesha maadili na imani.Imani haipatikani hivi hivi tu.
Mada hiyo hiyo inashadidiwa na gazeti la "Südwest-Presse" la mjini Ulm" na kuandika:
"Tunabidi turejirejeshee hali ya kuaminika".Hayo ni matamshi ya Philipp Rösler aliyoyatoa kwa hali ya utulivu-katika wakati ambapo changamoto kubwa kabisa inawasubiri watakaochaguliwa kukiongoza chama hicho cha kiliberali.Sera yao ya kupigania zaidi masoko haivutii tena.Wanahitaji mkakati wa aina mpya.FDP na hasa na aliyekuwa mwenyekiti hadi sasa wamekosea pakubwa walipojigeuka kuwa chama kinachopigania peke kodi za mapato zipunguzwe.
Mada yetu ya mwisho magazetini inahusiana na azma ya rais Barack Obama ya kugombea tena wadhifa huo.Gazeti la "Rhein-Zeitung" linaandika:
Barack Obama atalazimika kutetea vita ambavyo havipendwi nchini mwake.Atabidi awaeleze wamarekani waliovunjika moyo,kwanini wanasiasa mjini Washington wanatanguliza mbele malumbano ya kisiasa badala ya njia za busara za kuyapatia ufumbuzi matatizo yaliyopo.Na hilo hasa ndilo aliloahidi kulisawazisha.Hali imezidi kuharibika hivi sasa-ingawa makosa si yake,yanatokana na msimamo mkali wa upande wa upinzani wa kihafidhina.Lakini raia wa kawaida,hamjui mwengine isipokua yeye.Kwa maneno mengine;mapambano hayatakuwa rahisi mwakani.Hata hivyo Obama anafanya vizuri kuonyesha unyenyekevu.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/Inlandspresse
Mhariri:Abdul-Rahman