1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upigaji kura wachelewa Kwale

9 Agosti 2022

Wapiga kura katika kaunti ya Kwale pwani ya Kenya wamekumbwa na changamoto ya kucheleweshwa kwa vifaa vya kupigia kura.

https://p.dw.com/p/4FKGw
Ballot boxes and voting materials at Nyali polling station in Mombasa
Picha: Halima Gongo/DW

Vilevile baadhi ya watu wamekamatwa na maafisa wa polisi baada ya kuonekana wakiwahonga wapiga kura wawapigie kura baadhi ya viongozi. Watu hao wamefikishwa katika vituo vya polisi wakisubiri kufunguliwa mashtaka.

Shughuli ya kupiga kura katika shule ya msingi ya Chai iliyoko eneo bunge la Matuga kaunti ya Kwale ilianza saa 12 alfajiri ya Jumanne.

Vifaa vya kupigia kura na baadhi ya maafisa wanaosimamia shughuli ya kupiga kura wa IEBC katika baadhi ya vituo vya Kwale wamechelewa kufika vituoni  hali iliyosababisha watu kujaa vituoni kupita kiasi.

Baadhi ya wapiga kura pia walikumbwa na changamoto ya kuyapata majina yao jambo lililowafanya baadhi yao kurudi majumbani bila kupiga kura.

Akina mama wajawazito, waliokuwa na watoto wachanga na watu wenye ulemavu walikuwa wanapishwa mbele kuepuka  mstari mrefu wa wapiga kura waliokuwa wamefika vituoni.

Kumekuwa na visa katika vituo vya kupigia kura vya Chai, Kinango na Mangwei vya watu waliokuwa wanawahonga wapiga kura ili waweze kuwapigia kura baadhi ya wagombea. Baadhi yao wamekamatwa na kufikishwa katika vituo vya polisi.

Maafisa wa polisi walikuwa wameshika doria, wengine walikuwa kwenye milango ya vituo wakiwaelekeza wapiga kura kuingia vituoni kwa mpangilio ili kuepuka msongamano.

Vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa saa 11 jioni saa za Afrika Mashariki. Na masanduku yote yenye kura yatawasilishwa katika vituo vya kuhesabia kura vya kaunti ya Kwale.