Upinzani Belarus wafanya maandamano ya mwishoni mwa juma
15 Agosti 2020Wakati upinzani ukiendelea kupata nguvu baada ya siku kadhaa za maandamano kuhusiana na uchaguzi wa rais unaobishaniwa uliofanyika Jumapili iliyopita , mgombea mkuu wa upinzani katika uchaguzi huo Svetlana Tikhanovskaya amewataka waungaji wake mkono kufanya maandamano tena mwishoni mwa juma hili.
Wamekusanyika mchana siku ya Jumamosi karibu na kituo kikuu cha treni cha Pushkinskaya katika mji mkuu Minsk kwa kumuenzi Alexander Taraikovsky , muandamanaji mwenye umri wa miaka 34 ambaye alifariki hapo siku ya Jumatatu na ambaye mazishi yake yanafanyika.
"Maandamano kwa ajili ya uhuru" yamepangwa kufanyika katikati ya Minsk kesho Jumapili, wiki moja baada ya uchaguzi huo unaobishaniwa kwamba Lukashenko mwenye umri wa miaka 65 anadai kuwa ameshinda kwa asilimia 80 ya kura.
Tikhanovskaya , mwenye umri wa miaka 37 ambaye ndio kwanza amejiingiza katika siasa na ambaye aligombea baada ya wagombea wengine wa upinzani pamoja na mume wake kufungwa, anamshutumu Lukashenko kwa kughushi kura na anadai ajiuzulu ili uchaguzi mpya uweze kufanyika.
Aikimbia nchi
Ameikimbia nchi hiyo siku ya Jumanne na kukimbilia nchi jirani ya Lithuania, akiwa pamoja, washirika wake wakisema amekuwa katika shinikizo kutoka kwa maafisa wa serikali, lakini siku ya Ijumaa alijitokeza akitoa wito wa kufanyika maandamano mwishoni mwa juma, "ya mkusanyiko wa amani" katika miji nchini kote.
Pia anataka maafisa wawajibike kutokana na ukandamizaji wa polisi dhidi ya waandamanaji baada ya uchaguzi ambapo ukandamizaji huo umeshuhudia zaidi ya watu 6,700 wakikamatwa.
Polisi wametumia risasi za mipira, mabomu ya kusitua na takriban katika tukio moja, risasi za moto zilitumika kuyatawanya makundi, ambapo mamia walijeruhiwa.
Maafisa wamethibitisha vifo viwili katika machafuko hayo, ikiwa ni pamoja na Taraikovsky ambae wanasema alifariki wakati kiripuzi kiliporipuka mkononi mwake wakati wa maandamano, na mtu mwingine aliyefariki akiwa mikononi mwa polisi baada ya kukamatwa katika mji wa kusini mashariki wa Gomel.
Waachiwa huru
Siku ya Ijumaa maafisa walianza kuwaachia mamia ya watu waliowakamata na wengi walitoka kutoka kizuwizini wakielezea madhila makubwa ya kupigwa na kuteswa.
Shirika la kutetea haki za binadamu Amnesty International limeshutumu, kile ilichoeleza kuwa ni "kampeni wa mateso nchini nzima pamoja na matendo mengine ya ukiukaji haki yanayofanywa na mafisa wa Belarus ambao wana nia ya kuzima maandamano ya amani kwa njia yoyote ile."
Kiongozi wa Belarus Alexander Lukashenko amesema leo Jumamosi (15.08.2020) anataka kuzungumza na kiongozi wa Urusi Vladimir Putin wakati maandamano nchini mwake yakiongezeka kuhusiana na uchaguzi ambao unabishaniwa. "Mapambano dhidi ya Belarus yanaongezeka. Tunahitaji kuwa na mawasiliano na Putin, rais wa Urusi , ili niweze kuzungumza nae sasa," Lukashenko alisema katika mkutano na maafisa wa serikali. "Kwasababu hii tayari ni kitisho sio tu kwa Belarus."