1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Belarus wapongeza hatua ya Ulaya kutotambua matokeo

Sylvia Mwehozi
20 Agosti 2020

Wanasiasa wa upinzani nchini Belarus wamepongeza hatua ya Umoja wa Ulaya ya kutotambua matokeo ya uchaguzi kutokana na kuenea kwa madai ya udanganyifu wa kura, wakati rais Lukashenko akitishia kuwashughulikia upinzani. 

https://p.dw.com/p/3hDdj
Weissrussland Minsk | Massenproteste | Belarus Proteste
Picha: picture-alliance/dpa/Sputnik/V. Tolochko

 

Kufuatia mkutano wake wa uzinduzi wajumbe wa baraza la uratibu lililoanzishwa na upinzani kwa ajili ya kusaidia kipindi cha mpito cha madaraka, walitoa wito kwa Umoja wa Ulaya na Urusi kuratibu mazungumzo baina ya serikali na raia.

Baraza hilo limepitisha azimio linalotaka kukomeshwa kwa vurugu dhidi ya maandamano ya amani, kuachiwa kwa wafungwa wote wa kisiasa pamoja na uchaguzi mpya. Olga Kovalkova, kiongozi wa upinzani na aliyekuwa meneja kampeni wa mgombea upinzani Sviatlana Tikhanouskaya amesema kwamba; Soma zaidi Je, Ulaya itaiwekea vikwazo Belarus?

"Baraza la uratibu linazingatia kwamba suluhisho pekee la kumaliza mgogoro wa kisiasa ni kuanza mara moja kwa mazungumzo na kuendeleza njia za kurudisha uhalali na uchaguzi mpya."

Wito huo umetolewa saa chache baada ya rais wa baraza la Ulaya, Charles Michel kudai kwamba viongozi 27 wa nchi wanachama wa umoja huo "hawatambui matokeo yaliyotangazwa na mamlaka za Belarus" katika uchaguzi uliopita.

EU Virtueller Gipfel Belarus Belgien Charles Michel
Rais wa Baraza la Ulaya Charles Michel Picha: Reuters/O. Hoslet

Akizungumza baada ya mkutano wa njia ya vidio baina ya wakuu wa nchi wanachama kujadili namna ya kushughulikia mgogoro wa Belarus, Michel amesema watu kadhaa wanaohusika katika ukiukaji wa haki za binadamu na udanganyifu wa kura watawekewa vikwazo.

Naye Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ambaye taifa lake linashikilia kijiti cha uenyekiti wa kupokezana wa muungano wa ulaya, pia amekemea matumizi ya nguvu dhidi ya waandamanaji. Rais wa Halmashauri ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen, aligusia kwamba muungano huo utaunga mkono hatua ya Lukashenko kuachia madaraka.

Lakini rais Lukashenko mwenyewe ameendelea kupuuzia wito wa kuachia ngazi. Amelieleza baraza la usalama la taifa kwamba viongozi wa nchi za magharibi wanapaswa kuzingatia matatizo yao wenyewe badala ya kuingilia hali ya kisiasa nchini mwake. "Kabla ya kutunyoshea kidole, wangezungumzia maandamano ya vizibao vya njano huko Paris na maandamano ya ghasia ya Marekani", alisema Lukashenko katika taarifa iliyorushwa na shirika la habari la taifa BeITA. Lukashenko ametishia kuwafungulia mashitaka viongozi wa upinzani na kuvitaka vikosi vya usalama kuzidisha nguvu dhidi ya maandamano yanayotishia utawala wake wa miaka 26.

Baada ya mkutano wa Jumatano, wajumbe wa baraza la upinzani wamesema watalenga kuanzisha mazungumzo na serikali ya kubadlishana madaraka. Mapendekezo yao yanagusia kuitishwa uchaguzi mpya wa rais utakaoandaliwa na tume mpya ya uchaguzi itakayochaguliwa na kutaka uchunguzi dhidi ya ukandamizaji wa waandamanaji.