1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani Comoro wataka matokeo ya urais yabatilishwe

17 Januari 2024

Viongozi wa upinzani visiwani Comoro wametaka matokeo ya uchaguzi wa urais kutangazwa kuwa batili baada ya Rais Azali Assoumani kuchaguliwa tena licha ya madai ya kuwepo kwa udanganyifu katika zoezi la upigaji kura.

https://p.dw.com/p/4bNd2
Azali Assoumani
Rais wa Comoro Azali AssoumaniPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

 

Wagombea watano wa upinzani walioshindana na Rais Assoumani katika uchaguzi huo uliofanyika siku ya Jumapili, wamesema wanataka matokeo ya urais yafutwe.

Malalamiko ya upinzani yanatokea huku vikosi vya usalama vikikabiliana kwa gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji waliopinga kuchaguliwa tena kwa Rais Azzali Assoumani, walipojaribu kufunga barabara katika mji mkuu.

Wasiwasi watanda visiwani Comoro baada ya Azali Assoumani kutangazwa mshindi katika uchaguzi wa rais

Kulitokea vurugu katika mitaa kadhaa ya mji mkuu Moroni baada ya matokeo ya uchaguzi wa urais kutangazwa.

Msemaji wa serikali Houmed Msaidie akizungumza na shirika la habari la AFP, ameushtumu upinzani kwa kuandaa maandamano.

Upinzani umepinga ushindi wa mtawala wa zamani wa kijeshi Assoumani na kuutaja uchaguzi wa Jumapili kama udanganyifu wa wazi.