Upinzani DR Kongo wamtaka Tshisekedi kuacha kuwachokoza
9 Juni 2023Misako hiyo ilifanyika katika makazi ya Moses Katumbi hapa Kinshasa na ya mshauri wake Salomon Idi Kalonda huko Lubumbashi.
Chama Ensemble pour la République kimeshutumu na kulaani kile kinachokielezea kuwa ni unyanyasaji zaidi na wa kupita kiasi unaoendeshwa na utawala wa Rais Tshisekedi ili kuwanyamazisha wapinzani. Na hivyo chama hicho kimetoa wito kwa WaKongo kuyapinga mambo hayo.
Soma pia: Marekani yaitaka Kongo kuheshimu haki ya kuandamana
"Ensemble pour la République inalaani unyanyasaji mwingi na wa kupita kiasi. Misako iliyofanywa katika makazi ya kiongozi wake na yale ya mshirika wake ambaye bado yupo kizuizini, huo ni unyanyasaji ambao unalenga tu kuwafunga midomo wapinzani na kuficha utovu wa madaraka iliyo hapa," alisema Katibu Mkuu wa Ensemble pour la République, Dieudonné Bolenge Tenge
Kauli hiyo imeungwa mkono pia na Chama PPRD cha Rais wa zamani Joseph Kabila kikikumbusha kwamba familia ya Kabila pia inalengwa na mambo ya aina hiyo. Ndivyo alivyoeleza Ferdinand Kambere, Naibu Katibu Mkuu wa PPRD akishutumu pia kile anachokielezea kuwa rekodi mbaya ya utawala wa Félix Tshisekedi.
Soma pia: Mazungumzo ya Rais Tshisekedi na wapinzani yakwama
"Viongozi wanaendelea kutoa wito wa kupinga na kuwa na umoja. Ni katika familia yetu ya kisiasa ndipo walianzia vitisho hivyo. Kumbuka yote yaliyosemwa kuhusu wanamgambo wa Mubondo ambao mamlaka ilijaribu kuwaunganisha na makao ya Kabila kule Kingakati na kusema ni lazima kuendesha msako Kingakati. Upinzani wao ni rekodi yao wenyewe ambayo ni machafuko."
Hayo yote yamejiri zaidi ya wiki moja baada ya Salomon Idi Kalonda, mshauri maalum wa Moses Katumbi kukamatwa. Idara ya ujasusi ya kijeshi inamtuhumu kwa kuwasiliana na waasi wa M23 pamoja na maafisa wa Rwanda kwa lengo la kuupindua utawala wa Rais Tshisekedi.
Jean Noel Ba-Mweze, DW, Kinshasa.