Upinzani Mali wasema utafanya kazi na wanajeshi
20 Agosti 2020Jumuiya ya Kiuchumi ya mataifa ya Afrika magharibi ECOWAS, ambayo inakutana kujadili mzozo huo, imesimamisha uanachama wa Mali, kufunga mipaka na kuzuwia uingiaji wa fedha katika nchi hiyo katika hatua ya kujibu uasi uliotokea siku ya Jumanne uliosababisha mapinduzi dhidi ya serikali ya rais Ibrahim Boubacar Keita.
Muungano unaofahamika kama M5-RFP kundi la upinzani lililokuwa linapinga utawala wa Keita limesema linafanyakazi pamoja na wanajeshi waliofanya uasi, na kuviita vikwazo vilivyowekwa na jumuiya ya ECOWAS kuwa ni uchukuaji wa hatua bila kufikiria inayotokana na hofu ya baadhi ya viongozi wa kikanda kuwa mapinduzi yaliyofanyika yanaweza kuanzisha machafuko ya kisiasa katika nchi zao pia.
"Viongozi hao wanachukua msukumo kuiweka ECOWAS dhidi ya Mali," amesema msemaji wa kundi hilo la M5-RFP Nouhoum Togo.
"M5-RFP na CNSP ikiwa na maana kamati ya taifa ya uokozi wa umma, kwa hivi sasa zinafanyakazi kwa pamoja. Togo alisema benki zitafunguliwa na kufanyakazi kama kawaida leo Alhamis.Msemaji wa kamati ya mikakati ya M5-RFP Issa Kaou Djim amesema kila mtu atajumuishwa katika mchakato wa uongozi, wote ni watu wa Mali.
Hali ya maisha yaanza kurejea kawaida
Mji mkuu Bamako ulikuwa tulivu kwa siku ya pili mfululizo, siku moja baada ya shirika la habari la Reuters kusema, wakati watu wanaonekana kufuata miito ya msemaji wa uongozi wa jeshi kanali Ismael Wague wa kurejea kazini na kuendelea na maisha kama kawaida.
Mapinduzi hayo, ambayo yameitikisa nchi hiyo ambayo tangu hapo inakumbwa na mapigano ya makundi ya jihadi pamoja na machafuko ya umma, yamekumbana na shutuma kali kutoka jumuiya ya kimataifa.
Mapinduzi pia yamechochea wasi wasi kwamba yanaweza kuvuruga kampeni za kijeshi dhidi ya wapiganaji wa jihadi wenye mafungamano na kundi la al-Qaeda na kundi linalojiita Dola la Kiislamu yanayofanyakazi zao upande wa kaskazini na kati nchini Mali na eneo kubwa la Afrika magharibi la eneo la Sahel.
Wakuu wa mataifa 15 wanachama wa ECOWAS wanatarajiwa kujadili mapinduzi hayo katika kikao kwa njia ya vidio leo Alhamis.
Mwezi Julai , ujumbe kutoka kundi hilo la mataifa ulishindwa kupata makubaliano kati ya Keita na upinzani, ambao umeendesha maandamano makubwa dhidi ya serikali katika miezi ya hivi karibuni.
Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre
Mhariri: Iddi Ssessanga