Upinzani Msumbiji waitisha maandamano mapya
9 Novemba 2024Kiongozi wa upinzani Venancio Mondlane ambaye anasema matokeo ya uchaguzi huo yalichakachuliwa amewatolea mwito wafuasi wake kuteremka tena mitaani baada ya kufanya maandamano makubwa siku ya Alhamisi kwenye mji mkuu Maputo.
Maafisa wa usalama walitumia mabomu ya machozi na kutawanya mbwa wa polisi kuwakabili waandamanaji waliokuwa wakirusha mawe na kuweka vizuizi barabarani kwa kuchoma matairi na mapipa ya taka. Inaarifiwa kwamba watu 3 waliuawa kwnye ghasia hizo za Alhamisi na wengine 66 wamelazwa hospitali kutokana na majeraha.
Rais Filipe Nyusi anayeondoka madarakani aliwatembelea majeruhi hospitali na kuurai upande wa upinzani kuachana na vurugu na kugeukia meza ya mazungumzo.
Machafuko ya kisiasa nchini humo yalianza baada ya kutangazwa matokeo na makundi ya haki za binadamu yanasema hadi sasa takribani watu 30 wameuwa kwenye vurumai inayoshuhudiwa.