Upinzani waapa kutoshiriki katika uongozi Sierra Leone
1 Julai 2023Chama cha All Peoples Congress - APC kimesema kinakataa matokeo yaliyotangazwa, ikizingatiwa dosari na ukiukaji wa taratibu zilizowekwa za uchaguzi.
Kimetoa msururu wa masharti, ikiwemo kujiuzulu kwa makamishena wa uchaguzi, kikiwatuhumu kwa upendeleo na kushindwa kufanya majukumu yao pasina kuegemea upande wowote.
Soma pia: Rais wa Sierra Leone aongoza matokeo ya uchaguzi
Aidha kimetaka uchaguzi uandaliwe upya katika miezi sita, kikisema zoezi hilo lazima lisimamiwe na watu wenye uadilifu na taasisi zitakazohakikisha mchakato wa haki na wazi.
Rais Julius Maada Bio alichaguliwa tena kwa muhula wa pili katika duru ya kwanza ya upigaji kura akiwa na asilimia 56.17 ya kura. Chama cha APC kikiongozwa na kiongozi wake Samura Kamara kilikuwa cha pili na asilimia 41.16 ya kura.