Upo uwezekano wa Le Pen kushinda?
5 Mei 2017Kwa mujibu wa utafiti wa wapiga kura, Emmanuel Macron mwenye umri wa miaka 39 na asiye na chama, anatarajiwa kupata asilimia 62 ya kura huku ikitabiriwa kwamba mpinzani wake Marine Le Pen, atapata asilimia 38. Lakini swali kubwa lililopo kwa sasa ni iwapo Marine Le Pen bado ataweza kunyakua ushindi wa kushangaza. Ni swali ambalo wachambuzi na wataalamu wa siasa hawawezi kulijibu kwa uhakika. Wanaamini kwamba iwapo watu wachache watajitokeza kupiga kura, Marine Le Pen atafaidika.
Le Pen anaendesha kampeni zake kama alivyofanya Rais wa Marekani, Donald Trump. Anawaeleza Wafaransa kuwa nchi yao iko kwenye hali mbaya, huku akijitangaza mwenyewe kuwa mkombozi wa wananchi. Ahadi yake ni kurejesha tena ukaguzi wa watu wanaovuka mpaka kuingia Ufaransa, kupandisha kiwango cha ushuru wa forodha, kuitoa Ufaransa katika nchi zinazotumia sarafu ya Euro na ikiwezekana hata kuitoa Ufaransa kabisa kwenye Umoja wa Ulaya.
Ufaransa chini ya Le Pen itakuwa na sura gani?
Vivien Pertusot wa Taasisi ya Ufaransa ya Uhusiano wa Kimataifa anaelewa kwanini Le Pen ameweza kupata wafuasi wengi hivyo: "Hofu ya watu kuhusu utandawazi unaoathiri maisha yetu na usiodhibitika inaongezeka. Umoja wa Ulaya unachukuliwa kuwa adui, kwani unaruhusu watu kusafiri bila kujali mipaka ya nchi, bidhaa kuingia nchini bila ushuru na watu kuwa na uhuru wa kufanya kazi kwenye nchi yoyote. Hii inawapa watu hisia kwamba hawawezi kuamua mambo yanayofanyika nchini kwao."
Frank Baasner, Mkurugenzi wa Taasisi ya Uhusiano kati ya Ujerumani na Ufaransa, anaamini kwamba Ufaransa inayoongozwa na Marine Le Pen itajikuta kwenye matatizo makubwa: "Kama Le Pen atashinda, Ufaransa itapata shida. Itatengwa na nchi nyingine iwapo Le Pen atatimiza hata nusu tu ya ahadi zake za kampeni, kama vile kujitoa kwenye Umoja wa Ulaya. Mimi ninahofia kwamba kunaweza kukatokea vurugu na machafuko ya ghafla Ufaransa."
Emmanuel Macron kwa upande wake anasisitiza umuhimu wa Ufaransa kuwa sehemu ya Umoja wa Ulaya na moja ya nchi zinazotumia sarafu ya Euro. Vituo vya kupigia kura vitafungwa Jumapili saa mbili usiku kwa saa za Ufaransa na matokeo ya awali yatatangazwa mara baada ya hapo. Uchaguzi wa bunge utafanyika mwezi wa sita mwaka huu.
Mwandishi: Bernd Riegert
Tafsiri: Elizabeth Shoo
Mhariri: Iddi Ssessanga