Ureno kuisadia Msumbiji kupambana na waasi
14 Desemba 2020Waziri wa Ulinzi wa Ureno, Joao Gomes Cravinho amesema ana uhakika kwamba mwanzoni mwa mwaka 2021watafanikiwa kuanzisha ushirikiano ambao utaruhusu Msumbiji kutekeleza kikamilifu uhuru wake katika eneo lake lote.
Gomes amesema mazungumzo na viongozi wa Msumbiji yaliyofanyika wiki iliyopita, yalikuwa mazuri na ya kivitendo. Anasema wamezungumzia jinsi ya kufanya kazi pamoja.
Amani ya Msumbiji muhimu
Waziri huyo ambaye nchi yake itachukua urais wa kupokezana wa Umoja wa Ulaya mwezi Januari, amesema msaada huo utahusisha utoaji wa mafunzo na vifaa ili Msumbiji iweze kufanya kilicho muhimu kutafuta amani kwenye jimbo la Cabo Delgado lililoko kaskazini mwa Msumbiji.
Wanamgambo wenye mafungamano na kundi linalojiita Dola la Kiislamu wameongeza mashambulizi mwaka huu Cabo Delgado, ambako kuna utajiri wa gesi yenye thamani ya takriban dola bilioni 60. Wapiganaji hao wa jihadi mara kwa mara wamekuwa wakiwakamata wanajeshi na kuidhibiti miji kadhaa.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, watu 2,400 wameripotiwa kuuawa na mamilioni wameyakimbia makaazi yao kutokana na mashambulizi hayo.
Soma zaidi: Marekani kuisaidia Msumbiji kupambana na uasi
Wakati huo huo, Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi, UNHCR, limesema takriban watu 400,000 wameyakimbia mashambulizi hayo ya wanamgambo. Shirika hilo limeonya kuwa mzozo huo unaweza kuenea haraka nje ya mipaka ya nchi hiyo, iwapo nchi jirani za kikanda hazitaonesha juhudi za kusaidia kukabiliana na uasi.
Valentin Tapsoba, mkuu wa UNHCR kusini mwa Afrika, anasema familia ambazo zilikuwa zinaanzisha tena maisha yao baada ya uharibifu ulitokana na kimbunga Kenneth mwaka 2019, zimelazimika kuyakimbia mashambulizi hayo.
Idadi ya wakimbizi inaweza kuongezeka
Tapsoba amesema watu 424,000 wameyakimbia mashambulizi kwenye maeneo ya Niassa, Nampula na Pemba na idadi hiyo inaweza kuongezeka. Amesema maafisa wa Msumbiji wanaitaja idadi ya watu waliokimbia kuwa 570,000.
Msemaji wa rais wa Zimbabwe, George Charamba, amesema viongozi wa Msumbiji, Zimbabwe, Afrika Kusini, Botswana na Tanzania wanatarajiwa kukutana leo mjini Maputo kulizungumzia suala hilo.
Tapsoba amebainisha kuwa Ijumaa ijayo serikali ya Msumbiji pamoja na mashirika ya Umoja wa Mataifa pamoja na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali ya nchi hiyo, yatazindua ombi la kimataifa kuchangia fedha kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaokimbia mapigano Cabo Delgado.
UNHCR imechangisha robo ya dola milioni 19.2 zinazohitajika kwa ajili ya makaazi, chakula, maji na usafi wa mazingira kwa ajili ya matumizi ya mwaka ujao wa 2021.
Aidha, Shirika la Umoja wa Mataifa la Wahamiaji, IOM, limesema idadi kubwa ya wazee na watu wasiojiweza hasa kutoka kwenye wilaya za Cabo Delgado hawawezi kufikiwa na misaada ya kiutu na wanataka kukimbia. Afisa wa IOM, Sascha Nlabu amesema watu hao wanakabiliwa na vizuizi vya kutembea, kupata usafiri na nauli.
(AFP, Reuters)