Urusi na Iran kutia saini mkataba mpya wa ushirikiano
17 Januari 2024Mwezi uliopita, Putin alifanya mazungumzo yaliyodumu kwa saa tano katika ikulu ya Kremlin na Ebrahim Raisi katikati ya ongezeko la ushirikiano wa kisiasa, kibiashara na kijeshi kati ya Moscow na Tehran, ushirikiano ambao unawatia wasiwasi Marekani na Israel.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Urusi Maria Zakharov amewaambia waandishi wa habari kwamba, makubaliano hayo yataimarisha ushirikiano wa kimkakati kati ya Moscow na Tehran.
Bi. Zakharov amesema tangu kusainiwa kwa mkataba wa sasa, mazingira ya kimataifa yamebadilika na kwamba uhusiano kati ya Iran na Urusi umeendelea kuimarika.
Mamlaka ya Iran imeeleza kuwa ushirikiano wa kijeshi kati yake na Urusi unazidi kuwa mzuri kila siku. Iran ilisema mwezi Novemba kwamba ilikamilisha mipango na Urusi ya kuipa ndege za kivita aina ya Su-35 na helikopta aina ya Mi-28.