1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroUkraine

Urusi na Ukraine zashambuliana kwa makombora

20 Desemba 2024

Makombora ya masafa marefu ya Urusi yameupiga mji mkuu wa Ukraine, Kyiv mapema leo na kumuuwa mtu mmoja na kuwajeruhi wengine tisa.

https://p.dw.com/p/4oPUL
Ukraine | Urusi | Kherson
Jengo lililoharibiwa kufuatia shambulio la anga la Urusi eneo la KhersonPicha: Kherson Regional Military Administration/Anadolu/picture alliance

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema shambulizi hilo lilikuwa la kujibu shambulizi la kombora la Ukraine kwenye ardhi ya Urusi kwa kutumia silaha zilizotengenezwa Marekani.

Maafisa wa Kyiv wamesema shambulizi hilo la alfajiri liliharibu mfumo wa kupasha joto majumbani na kuyaathiri majengo 630, vituo vya afya 16 na shule 30 zikiwemo za chekechea.

Soma pia: Urusi yapuuza sheria ya kudhibiti silaha

Urusi imesema Ukraine ilitumia makombora sita aina ya ATACMS ya kutengenezwa na Marekani na manne aina ya Storm Shadow ya kufyatuliwa kutoka angani ambayo yanatolewa na Uingereza.

Shambulizi hilo la Ukraine mapema leo liliupiga mkoa wa Urusi wa Rostov. Matumizi ya silaha zinazotolewa na nchi za Magharibi kuyashambulia maeneo ndani ya Urusi yameikasirisha serikali ya Urusi.

Wizara ya Ulinzi ya Urusi imesema imelipinga jengo la kamandi ya shirika la ujasusi la Ukraine - SBU mjini Kyiv, ambalo imesema linahusika katika kuyatengeneza makombora, pamoja na mfumo wa ulinzi wa makombora ya kurushwa kutokea angani.