1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi: NATO yaandaa mazingira ya Vita vya Tatu vya Dunia

26 Aprili 2022

Urusi imeutuhumu muungano wa kujihami wa NATO kwa kile inachosema ni kuweka mazingira ya kuanza kwa vita vya nyuklia kwa kuipatia Ukraine zana za kivita.

https://p.dw.com/p/4AT1O
Lawrow sieht "reale Gefahr" eines dritten Weltkrieges
Picha: Attila Kisbenedek/AFP/Getty Images

Urusi imeyasema haya wakati Marekani na marafiki zake wamekutana mjini Ramstein nchini Ujerumani Jumanne kutoa ahadi ya silaha nzito inazohitaji Ukraine ili iweze kupata ushindi katika mapambano yake na Urusi.

Katika mwendelezo wa matamashi makali yanayoendelea kutolewa na Urusi, waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo Sergei Lavrov alipoulizwa katika televisheni ya kitaifa nchini Urusi kuhusiana na uwezekano wa kuzuka kwa Vita vya tatu vya Dunia amesema "ipo hatari ya hilo kufanyika na hatari yenyewe ni kubwa kwa kuwa muungano wa NATO uko katika vita vya kiwakala na Urusi na muungano huo unamuhami huyo wakala, kwa hiyo vita ni vita."

Misaada zaidi ya kijeshi kuelekea Ukraine

Wiki hii Marekani imeondoa msisitizo wake kutoka ule wa kutaka kuisaidia Ukraine ijilinde na sasa inazungumzia suala la ushindi wa Ukraine kama njia ya kuizuwia Urusi isiendelee kuwatishia majirani zake.

Waandamanaji Ujerumani wataka kusitishwa ununuzi gesi Urusi

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Lloyd Austin Jumanne ameiahidi Ukraine kuwa msaada zaidi wa kivita upo njiani wakati alipofanya mkutano na maafisa wa nchi 40 kutoka nchi tofauti duniani katika kambi ya kijeshi ya Ramstein nchini Ujerumani. Ni katika mkutano huo ambapo Ujerumani ambayo imekuwa na sera ya tahadhari katika vita hivi, imeahidi kutuma zana nzito kwa Ukraine.

Haya yanafanyika wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov amesema kuwa Urusi iko tayari kushirikiana na Umoja wa Mataifa kuwasaidia raia nchini Ukraine ambapo Urusi imekuwa ikifanya operesheni ya kijeshi kwa zaidi ya miezi miwili sasa.

Kauli hii ya Lavrov imekuja baada ya kukutana na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres mjini Moscow Jumanne ambapo mkuu huyo wa Umoja wa Mataifa amependekeza kuanzishwa ushirikiano wa pande tatu, Umoja wa Mataifa, Urusi na Ukraine ili kutatua matatizo ya kiutu nchini Ukraine.

"Na tunahitaji kwa haraka njia za misaada ya kiutu ambazo zinafanya kazi, ni salama na zinaheshimiwa na kila mmoja ili kuwaokoa raia na kuwasilisha misaada inayohitajika mno," alisema Guterres.

Hofu katika nchi za mashariki mwa Ulaya

Kulingana na Lavrov, Guterres atakutana pia na Rais Vladimir Putin. Viongozi hawa wanakutana huku Urusi ikiwa bado inaendeleza mashambulizi yake kusini na mashariki mwa Ukraine ambapo maafisa wanasema watu tisa wameuwawa Jumanne kufuatia mashambulizi ya mabomu katika mji wa Kharkiv.

Russland Moskau UN Generealsekretär Antonio Guterres
Mkuu wa UN Antonio Guterres (kushoto) na Sergei Lavrov wa Urusi (kulia)Picha: Maxim Shipenkov/REUTERS

Uvamizi wa Urusi umezitia hofu nchi kadhaa mashariki mwa Ulaya zinazohofia kuwa huenda ndizo zitakazofuata baada ya Ukraine.

Wasiwasi huo umeongezeka nchini Moldova baada ya kamanda mmoja wa Urusi kusema kuidhibiti Ukraine kusini kutafungua njia ya kuelekea eneo la Trans-Dniester linalotaka kujitenga nchini Moldova.

Chanzo: Reuters/AFP/DPA