Urusi, Ukraine zabadilishana wafungwa
22 Septemba 2022Kubadilishana kwa wafungwa hao kulihusisha karibu watu 300, wakiwemo raia 10 wa kigeni na makamanda walioiongoza oparesheni ya kijeshi katika eneo la Mariupol mapema mwaka huu.
Wafungwa wa kigeni walioachiliwa huru ni pamoja na Waingereza wawili na raia mmoja wa Morocco ambaye alikuwa amehukumiwa kifo mnamo mwezi Juni baada ya kukamatwa akiwasaidia wanajeshi wa Ukraine katika uwanja wa mapambano. Wengine walioachiliwa ni Wamarekani wawili, raia mmoja wa Croatia na mwengine wa Uswidi.
Soma pia: Biden amkosoa Putin, ataka mageuzi Umoja wa Mataifa
Hata hivyo, muda na ukubwa wa hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa ndio imewashangaza wengi hasa ikizingatiwa kuwa rais wa Urusi Vladimir Putin alikuwa ametangaza uhamasishaji wa vijana kujiunga na kikosi cha jeshikatika hali ambayo inatishia kuongezeka kwa mzozo huo ulioanza mwezi Februari.
Makundi ya wapiganaji na wanaoungwa mkono na Urusi walisema mwezi uliopita kuwa makamanda wa Mariupol watapandishwa kizimbani.
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenksy amesema hatua hiyo ya kubadilishana wafungwa- ambayo ilihusisha mazungumzo kutoka Uturuki na Saudi Arabia- ilikuwa inafanyiwa kazi kwa muda mrefu.
Chini ya masharti ya makubaliano hayo, Waukraine 215- ambao wengi wao walikamatwa baada ya eneo la Mariupol kuwa chini ya udhibiti wa vikosi vya Urusi, waliachiliwa.
Kwa upande wa Ukraine, Kiev iliwarudisha Warusi 55 na raia kadhaa wa Ukraine wanayoiunga mkono Moscow pamoja na Viktor Medvedchuk, kiongozi wa chama kinachoungwa mkono na Urusi na ambacho kilikuwa kimepigwa marufuku. Medvedchuk alikuwa anakabiliwa na mashtaka ya uhaini.
Soma pia: Warusi wakimbia baada ya tangazo la uhamasishaji wa kijeshi
Katika ujumbe kwa njia ya video, Zelenksy amesema na hapa namnukuu, "Huu ni ushindi kwa nchi yetu na jamii yetu kwa ujumla. Lakini jambo la msingi ni kwamba familia 215 zitapata nafasi ya kuonana na wapendwa wao wakiwa salama nyumbani."
Zelenksy alitoa shukrani kwa rais wa Uturuki Tayyip Erdogan kwa mkono wake katika kufanikisha hilo. Rais huyo wa Ukraine amesema kuwa Makamanda hao wa Ukraine watasalia Uturuki hadi mwisho wa vita hivyo.
Ameeleza kuwa umekuwa mchakato mrefu wenye panda shuka tele katika kuhakikisha raia hao wa Ukraine wanaachiliwa huru. Miongoni mwa walioachiliwa ni Luteni Kanali Denys Prokopenko, Kamanda wa jeshi wa kikosi cha Azov, naibu wake Svyatoslav Palamar. Mwengine aliyeachiliwa ni kamanda wa jeshi la wanamaji Serhiy Volynsky.