Urusi yaandaa mashambulizi mapya dhidi ya Ukraine
26 Februari 2024Akizungumza baada ya maadhimisho ya pili tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Zelenskiy amesema ni muhimu kwa Kyiv na washirika wake wa Magharibi kuendelea na mshikamano na kusisitiza kwamba ushindi wa Ukraine unategemea ungwaji mkono wa kuendelea na nchi za Magharibi.
Zelenskiy amekiri kwamba wanajeshi 31,000 wa Ukraine wameuwawa tangu Februari 2022, akitoa takwimu rasmi za kwanza kwa zaidi ya mwaka mmoja. Hata hivyo Wizara ya mambo ya nje ya Urusi haikubaliani na takwimu za Ukraine na kuongeza kwamba ni za uongo.
"Wanajeshi 31,000 wa Ukraine walikufa katika vita hivi. Sio 300,000 sio 150,000 ambazo Putin alisema uwongo. Lakini hata hivyo, kila moja ya hasara hizi ni kujitolea kwa ajili yetu."
"Wanajeshi wa Urusi 180,000 pia wameuwawa, hasara ya jumla, waliokufa na waliojeruhiwa ni 180,000, sijui ni wangapi waliokufa na waliopotea, lakini najua ni hadi nusu milioni pamoja na wale waliojeruhiwa."
Zelensky ameongeza kusema "Ukraine ni 31,000 na ni uchungu sana. Sitasema idadi ya waliojeruhiwa kwa sababu Urusi itajua ni watu wangapi wameondoka kwenye mstari wa mbele wa mapambano.”
Ripoti ya gazeti la New York Times mwezi Agosti iliwanukuu maafisa wa Marekani ambao wanataja idadi ya vifo vya Ukraine kuwa takriba 70,000 na upande wa Urusi takriban wanajeshi 120,000 wameuwawa katika vita hivyo.
Takwimu hizo hata hivyo hazikuweza kuthibitishwa kwa kujitegemea kwani Urusi na Ukrainia mara nyingi imepuuza idadi ya vifo vya wanajeshi wao katika vita, huku wakitia chumvi hasara wanayodai kusababisha kwa upande pinzani.
Mashambulizi yaendelea kurindima
Zelenskyy pia amezungumza kuhusu mapigano yanayoendelea kaskazini-mashariki mwa Ukraine, ambapo mzozo katika mstari wa mbele wa vita umeongezeka katika miezi ya hivi karibuni.
Katika wiki za hivi karibuni, wanajeshi wa Ukraine wamekabiliwa na uhaba wa risasi na makombora, baada ya mzozo katika bunge la Marekani kuhusu msaada wa kijeshi wa dola bilioni 60 kwa Kiev.
Soma pia: Nusu ya msaada wa Magharibi kwa Ukraine haukufika kwa wakati
Wiki iliyopita, wanajeshi wake walilazimika kuondoka katika mji wa mashariki wa Avdiivka katika jimbo la Donestk ambako hali inaripotiwa kuwa mbaya.
Azimio la Ulaya
Huku haya yakijiri baadi ya viongozi 20 wa Ulaya wamekusanyika mjini Paris leo Jumatatu, kutuma ujumbe kwa Rais wa Urusi Vladimir Putin kuhusu azimio la Ulaya katika kuiunga mkono Ukraine na kupinga hoja ya Kremlin kwamba Urusi itashinda vita hivyo.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron amewaalika viongozi hao katika kasri la Elysee kwa mkutano wa ghafla kwa sababu ya kile ambacho washauri wake wanasema ni kuongezeka kwa uvamizi wa Urusi katika wiki chache zilizopita.
Soma pia:Macron aihimiza Ulaya kuharakisha msaada kwa Ukraine
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa Poland Andrzej Duda watakuwa miongoni mwa wakuu wa nchi na serikali 20 wa Ulaya watakaohudhuria mkutano huo utaoendeshwa pia kwa njia ya video na kufunguliwa rasmi kwa hotuba kutoka kwa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky.
Reuters//AFP