Urusi yadai kumzuilia mshukiwa aliyemuua Igor Kirillov
18 Desemba 2024Kwenye taarifa, kamati ya Uchunguzi ya Urusi inayochunguza matukio makubwa ya jinai, imesema mshukiwa huyo ambaye hajatambulishwa jina aliwaambia kwamba alienda Moscow kutekeleza shambulizi hilo kwa niaba ya vikosi vya ujasusi vya Ukraine.
Kwenye kanda ya vidio iliyorekodiwa akikiri kuhusika kwake na iliyochapishwa na shirika la habari la Baza, na linalofahamika kuwa na vyanzo vya habari ndani ya vyombo vya usalama vya Urusi, mshukiwa huyo alionekana akiwa ameketi ndani ya gari akisimulia matendo yake.
Unaweza kusoma Russia: Jenerali wa ulinzi wa nyuklia Igor Kirillov auawa
Haikubainika wazi alikuwa katika mazingira au hali gani alipokuwa akisimulia matukio hayo na shirika la habari la Reuters halikuweza kuihakiki vidio hiyo mara moja.
Mshukiwa anaonekana akisema alishauriwa kununua baiskeli ya umeme kisha miezi michache baadaye alipewa kilipuzi na majasusi wa Ukraine ili kutekeleza mpango huo.
Alielezea jinsi alivyokiweka kifaa hicho cha kulipuka kwenye baiskeli hiyo aliyoiegesha nje ya mlango wa jengo alikoishi Kirillov.
Urusi yasema mshukiwa aliahidiwa $100,000 na kuishi Ulaya
Wachunguzi walimnukuu akisema aliweka kamera ya uchunguzi juu ya gari lililokuwa karibu na eneo la mkasa na hivyo kuwawezesha majasusi wa Ukraine waliopanga njama hiyo kutizama hali halisi wakiwa Ukraine.
Unaweza kusoma pia: Trump aahidi tena kumaliza "mauaji" ya vita vya Ukraine
"Mshukiwa anaendelea kuchjunguzwa. Wakati wa kuhojiwa, alieleza kwamba alikuwa ameajiriwa na shirika la ujasusi la Ukraine. Kufuatia maagizo yao, alifika Moscow na kupokea kifaa cha kulipuka. Aliiweka kwenye baiskeli ya umeme, ambayo aliiegesha kwenye mlango wa jengo la ghorofa ambalo Igor Kirillov aliishi," amesema Svetlania Petrenko, msemaji wa kamati ya uchunguzi ya Urusi.
Kwenye kanda hiyo, mshukiwa huyo aliyezaliwa mwaka 1995 anasema aliilipua bomu hilo punde tu Kirillov alitoka nje ya jengo.
Kulingana na vidio hiyo, mshukiwa amesema aliahidiwa dola 100,000 kwa kazi hiyo ya kumuua Kirillov na pia alihakikishiwa nafasi ya kuishi katika taifa la Ulaya.
Uchunguzi zaidi kukamata washukiwa zaidi waendelea
Wachunguzi wamesema wanaendelea kuwatambua watu wengine waliohusika kwenye shambulizi hilo huku jarida la kila siku Kommersant la nchini Urusi likisema mshukiwa mwengine pia tayari anashikiliwa. Shirika la Habari la Reuters halikuweza kuthibitisha hilo.
Kirillov aliyekuwa mkuu wa kitengo cha ulinzi dhidi ya zana za nyuklia, kemikali na baolojia, aliuawa nje ya nyumba yake pamoja na msaidizi wake, baada ya bomu lililotegwa kwenye baiskeli ya umeme kulipuka mapema Jumatano.
Yeye ndiye afisa wa ngazi ya juu zaidi wa Urusi kuuawa na Ukraine ndani ya Urusi kufuatia mzozo huo wa Urusi na Ukraine ulioanza Februari 2022. Shirika la intelijensia la Ukraine SBU lililomtuhumu Kirillov kuhusika na mashambulizi dhidi ya vikosi vya Ukraine kutumia silaha za kemikali, lilikiri kuhusika na shambulizi hilo.
Urusi yamfunga raia wake mmoja miaka 20 jela
Katika tukio tofauti, mahakama ya kijeshi ya Urusi imemhukumu raia wake mmoja kifungo cha miaka 20 jela, kwa kujaribu kuwaua wanajeshi wa Urusi kwa njia ya sumu na pia kwa kuunga mkono Ukraine. Hayo ni kwa mujibu wa shirika la kiusalama nchini humo FSB.
Tukiachana na hayo, Urusi imesema itatoa jibu dhidi ya vikwazo vipya ilivyowekewa na Umoja wa Ulaya. Kulingana na msemaji wa wizara yake ya mambo ya kigeni Maria Zakhjarova, vikwazo hivyo ni hatari kwa usalama wa nishati kote ulimwenguni.
Mnamo Jumatatu, Umoja wa Ulaya ulitangaza vikwazo vipyakwa mara ya kumi na tano dhidi ya Urusi, ikiwemo masharti makali kwa kampuni za China na dhidi ya meli zaidi kutoka Urusi.
(RTRE; AFPE)