1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Urusi yaijibu Marekani kwa kuwatimua wanadiplomasia wake

17 Aprili 2021

Urusi imewataka wanadiplomasia 10 wa Marekani kuondoka nchini humo katika hatua ya kulipiza kisasi baada ya Marekani kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Urusi kwa madai ya udukuzi na kuingilia uchaguzi wa Marekani.

https://p.dw.com/p/3s9L4
USA Russland Kombo Joe Biden und Putin
Picha: Eric Baradat/Pavel Golovkin/AFP

Urusi imewataka wanadiplomasia 10 wa Marekani kuondoka nchini humo katika hatua ya kulipiza kisasi baada ya Marekani kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Urusi kwa madai ya udukuzi na kuingilia kati uchaguzi wa Marekani wa mwaka uliopita.

Wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema John Sullivan, ambaye ni balozi wa Marekani nchini Urusi, anapaswa kurudi nyumbani katika kile walichosema ni kwa mashauriano zaidi.

US-Botschafter John J. Sullivan
Balozi wa Marekani nchini Urusi John SullivanPicha: Mikhail Metzel/TASS/dpa/picture alliance

Kupitia taarifa, wizara ya mambo ya nje ya Urusi imesema huu ni wakati wa Marekani kuonyesha ukomavu wake wa kiakili na kugeuza mkondo wao wa kugombana.

Taarifa hiyo imeongeza kusema kuwa ina uwezo wa kuiumiza zaidi Marekani kuichumi na kupunguza idadi ya wanadiplomasia wa Marekani nchini Urusi hadi 300, japo kwa sasa haitachukua hatua hiyo.

Soma zaidi:Urusi yajitetea kujiimarisha kijeshi kwenye mpaka na Ukraine

Uamuzi wa Urusi, ukiwa sehemu ya mpango mpana wa kulipiza kisasi, uliidhinishwa na Rais Vladimir Putin kama jibu kwa Marekani baada ya serikali ya Joe Biden kuiwekea vikwazo Urusi.

Hata hivyo licha ya Moscow kujibu kwa haraka na kuweka hatua ambazo zinanuia kupunguza ushawishi wa Marekani nchini Urusi, Urusi imeacha mwanya wa mazungumzo uliopendekezwa na Rais Joe Biden aliyetaka kufanyika mkutano kati yake na Putin ili kujadili masuala kadhaa.

Marekani imeituhumu Urusi kwa udukuzi na kuingilia uchaguzi wake

Washington Außenministerium Rede USA Außenpolitik Biden
Picha: Saul Loeb/AFP/Getty Images

Marekani imesema vikwazo ilivyoiwekea Urusi ni jibu lake kwa Urusi baada ya Moscow kuingilia uchaguzi wa mwaka jana wa Marekani, kufanya udukuzi, na kuitishia Ukraine pamoja na vitendo vyengine.

Hata hivyo, Urusi imekanusha madai yote dhidi yake.

Vile vile, Ikulu ya Kremlin imesema Rais Putin bado hajaamua iwapo atashiriki katika mkutano wa kujadili athari za mabadiliko ya tabia nchi unaoongozwa na Marekani wiki ijayo.

Kremlin pia imeongeza kusema, itakuwa vigumu kuandaa kwa haraka mkutano wa kilele baina ya Putin na Biden.

Msemaji wa Ikulu Dmitry Peskov alisema jana Ijumaa kuwa Putin kwa muda mrefu amezungumzia juu ya umuhimu wa kurejesha uhusiano wa kawaida kati ya Marekani na Urusi.

Peskov alisema "Ni vizuri kuwa viongozi hao wawili wamekubaliana juu ya hili." Hata hivyo, msemaji huyo ameshtumu vikwazo vipya vilivyowekwa na Marekani, akisema "uraibu wa vikwazo vya Marekani haukubaliki."

Uhusiano kati ya Urusi na Marekani umetetereka katika siku za hivi karibuni baada ya Rais Biden kusema kuwa anadhani Putin ni "muuaji" na Moscow kujibu kwa kumuita nyumbani balozi wake anayehudumu nchini Marekani mnamo mwezi Machi. Balozi huyo bado hajarudi Marekani karibu mwezi mmoja baadaye.