Urusi yakabiliana na Ukraine kwa siku ya tatu mfululizo
9 Agosti 2024Uvanmizi huu wa Ukraine dhidi ya Urusi unatajwa kuwa mkubwa kabisa kuwahi kufanyika tangu vita vianze mwezi Februari 2022.
Mapigano makali yameripotiwa karibu na mji wa Sudzha, ambako kuna mitambo ya kusafirisha gesi ya Urusi kuelekea Ukraine, jambo ambalo limezusha wasiwasi wa kusimamishwa kwa upelekaji nishati hiyo barani Ulaya.
Kaimu gavana wa mkoa wa Kursk, Alexei Smirnov, amesema maelfu ya raia wamehamishwa kutoka eneo hilo kwa ajili ya usalama wao.
Wakati huo huo, mapema leo, mamlaka nchini Urusi zimesema Ukraine imefanya mashambulizi makali ya ndege zisizo rubani katika mkoa mwengine wa Lipetsk ulio kwenye mpaka wake wa kusini magharibi.
Gavana wa mkoa huo, Igor Artamonov, amesema mfumo wa kutungua makombora umezidunguwa baadhi ya droni hizo. Rais Vladimir Putin ameyaita mashambulizi hayo kuwa ni uchokozi mkubwa, huku wanasiasa wengine wakiyaita kuwa ni mashambulizi ya kigaidi.