1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Urusi yaongeza mashambulio yake dhidi ya Ukraine

16 Mei 2023

Urusi imefanya mashambulizi makali ya anga dhidi ya Ukraine mapema alfajiri, lakini Ukraine imesema mifumo yake ya ulinzi wa anga imefanikiwa kuyaharibu makombora 18 yaliyorushwa na Urusi ikiwemo sita yenye kasi kubwa.

https://p.dw.com/p/4RPCF
Situation in Artyomovsk
Picha: Valentin Sprinchak/TASS/dpa/picture alliance

Ukraine imesema mifumo yake ya ulinzi iliyadungua makombora yote 18 yaliyokuwa yamefyetuliwa kuelekea mji mkuu Kiev.

Sauti ya miripuko mikubwa ilisikika katika mji huo kufuatia mashambulizi ya usiku iliyojumuisha makombora yaliyorushwa kutoka Urusi kutokea angani,baharini na ardhini katika kile ambacho huenda lilikuwa jaribio la kuuharibu mifumo ya ulinzi wa anga ya Ukraine.

Msemaji wa jeshi la anga la Ukraine Yurii Ihnat amesema miongoni mwa makombora yaliyorushwa yalikuwemo ya kurushwa kwa droni,yale ya masafa ya kati na yenye kasi kubwa na yote yalidunguliwa ikiwemo sita aina ya Kinzal yaliyofyetuliwa kutoka kwenye ndege ya kivita aina ya MiG-31K.

Hata hivyo hakuna kifo kilichoripotiwa ingawa mkuu wa shughuli za kijeshi mjini Kiev Serhii Popko amesema mashambulio hayo ya Urusi dhidi ya mji huo yalikuwa ya aina yake kwa kuzingatia  ukubwa wake pamoja na idadi ya makombora yaliyorushwa ndani ya kipindi kifupi.

Uharibifu mkubwa umeripotiwa katika mji huo wa kiev ikiwa ni pamoja na baadhi ya majengo kuteketea na magari kuharibiwa kwa majengo yaliyoporomoka.

Uingereza yasema mashambulio ya Urusi kwa Ukraine yanafanya hali kuendelea kuwa ngumu 

Ukraine Kiew | Britische Botschafterin Melinda Simmons
Balozi wa Uingereza nchini Ukraine Melinda Simmons Picha: Volodymyr Tarasov/Ukrinform/imago images

Balozi wa Uingereza nchini Ukraine Melinda Simmons katika ujumbe aliouandika kwenye ukurasa wake wa Tweeter ameyaeleza mashambulio hayo ya makombora ya Urusi kuwa makali akisema yalisababisha mirindimo mizito na kuta kutikisika na kuifanya hali usiku mzima kutokuwa rahisi.

Ni mara ya nane mwezi huu ambapo Urusi inashuhudiwa ikifanya mashambulizi yake ya anga yakiulenga hasa mji mkuu wa Ukraine Kiev. Inaelezwa kwamba  hali hiyo inaonesha waziwazi vita vinaongezeka baada ya wiki kadhaa za utulivu kiasi na katika wakati ambapo Ukraine inatarajiwa kuanzisha operesheni kubwa  ya kujibu mashambulizi ya Urusi.

Lakini pia mashambulizi ya Urusi yamekuja katika wakati ambapo rais Volodymr Zelensky amekamilisha ziara yake barani Ulaya iliyomfikisha kwa washirika wake muhimu kwenye vita hivi ambako amejizolea tena  ahadi nyingine ya kupewa msaada wa kijeshi.

Kadhalika mashambulio ya Urusi yamekuja wakati viongozi wa Ulaya wanatarajia kushiriki mkutano wa kilele wa  nchi 46 wanachama wa baraza la Ulaya,ambacho ni chombo kikuu barani humo kinachohusika na masuala ya haki za binadamu.

Mkutano huo wa siku mbili unafanyika IceLand na lengo lake ni pamoja na kutafuta njia ya kutazama uharibifu uliofanywa na jeshi la Urusi nchini Ukraine ili kuanzisha juhudi za kuitaka Urusi ilipe fidia

Chanzo: afp,ap, reuters

DW Kiswahili | Saumu Mwasimba
Saumu Mwasimba Mhariri na mtangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW