Urusi yapeleka wanajeshi Kazakhstan kutuliza vurugu
6 Januari 2022Kazakhstan ambayo ina utajiri wa nishati na kwa muda mrefu imechukuliwa kuwa mojawapo ya jamhuri zenye utulivu za uliokuwa Muungano wa Kisovieti katika eneo la Asia ya Kati, inakabiliwa na mgogoro wake mkubwa zaidi kuwahi kushuhidiwa katika miongo mingi baada ya siku kadhaa za maandamano kuhusu kuongezeka kwa bei za mafuta kugeuka na kuwa machafuko kote nchini humo.
Chini ya ongezeko la shinikizo, Rais Kassym-Jomart Tokayev jana usiku aliliomba Shirika la Mkataba wa Usalama wa Pamoja – CSTO, ambalo linalotawaliwa na Urusi na kujumuisha mataifa mengine matano ya uliokuwa muungano wa Kisovieti, kupambana na kile alichokiita kuwa ni "makundi ya kigaidi” ambayo "yalipewa mafunzo ya kutosha nje ya nchi”.
CSTO yasema ni uingiliaji wa kigeni
Baada ya saa kadhaa, muungano huo ukasema wanajeshi wa kwanza wametumwa, wakiwemo askari maalum wa Urusi na vikosi vya kijeshi kutoka kwa wanachama wengine wa CSTO. Mwenyekiti wa sasa wa CSTO Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan, awali alitangaza kuwa muungano huo utaridhia ombi hilo, akisema Kazakhstan inakabiliwa na "uingiliaji wa nje”.
Katika machafuko mabaya kabisa kuwahi kuhushudiwa mpaka sasa, polisi imesema watu kadhaa waliuawa katika mapambano na vikosi vya usalama katika majengo ya serikali kwenye mji wa mkubwa wa nchi hiyo wa Almaty. Ripoti za vyombo vya habari nchini humo zinasema maafisa 12 wa usalama wameuawa na 353 kujeruhiwa katika vurugu hizo.
Rais Tokayev amesema katika hotuba iliyorushwa kwenye televisheni mapema leo kuwa magaidi wanakamata majengo, miundo mbinu, na silaha ndogondogo, na kukabiliana na vikosi vya usalama.
Maafisa wamesema zaidi ya watu 1,000 wamejeruhiwa mpaka sasa huku karibu 400 wakilazwa hospital, na 62 katika vyumba vya wagonjwa wahututi.
Maandamano yalisambaa wiki hii kote katika nchi hiyo yenye watu milioni 19 kulalamikia kupandishwa kwa bei za petroli mnamo katika Siku Kuu ya Mwaka Mpya. Maelfu waliingia mitaani mjini Almaty na mkoa wa magharibi wa Mangystau wakisema ongezeko la bei sio haki ikizingatiwa kuwa utajiri wa Kazakhstan wa visima vya mafuta na gesi
Hali ya Hatari yarefushwa kote nchini
Maandamano hayo ni kitisho kikubwa mpaka sasa kwa serikali iliyoundwa na rais mwanzilishi wa Kazakhstan Nursultan Nazarbayev, aliyejiuzulu mwaka wa 2019 na kumteuwa Tokayev kuwa mrithi wake.
Tokayev alijaribu kutuliza joto kwa kutangaza kujiuzulu kwa serikali inayoongozwa na Waziri Mkuu Askar Mamin mapema jana, lakini maandamano yaliendelea.
Tokayev pia ametangaza kuwa amechukua usukani kutoka kwa Nazarbayev kama mkuu wa baraza la usalama. Huku maandamano yakiendelea, serikali imesema hali ya hatari iliyotangazwa katika maeneo yaliyoathiriwa na maandamano itarefushwa kote nchini hadi Januari 19.
Umoja wa Ulaya na Umoja wa Mataifa wametoa wito kwa pande zote kujizuia, wakati Marekani ikiiomba serikali kuwaruhusu waandamanaji kujieleza kwa njia ya amani.
AFP